















Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya Zanzibar (ZHSF), kimeandaa bonanza maalumu la michezo kwa lengo la kuwahamasisha wanafunzi kujiunga na mfuko huo ili waweze kupata huduma za afya kwa urahisi na kupunguza gharama za matibabu wanapokabiliwa na changamoto za kiafya.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa bonanza hilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Jamal Jumanne Athumani, amesema SUZA inajivunia kuwa chuo kinachojali ustawi wa wanafunzi wake, ikiwemo afya zao, sambamba na kuendeleza michezo mbalimbali chuoni hapo.
Prof. Jamal amewataka wanafunzi kutumia fursa za michezo kuonesha vipaji vyao, akisisitiza kuwa michezo si nyenzo ya kujenga afya na kuimarisha umoja pekee, bali pia ni fursa inayoweza kuwa chanzo cha ajira na kujipatia kipato. Aidha, amewahakikishia wanafunzi kuwa SUZA itaendelea kuratibu mashindano mbalimbali na kuandaa zawadi kwa washindi ili kuongeza hamasa na ushindani miongoni mwa washiriki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ustawi wa Wanafunzi SUZA, Ndugu Salha Khalfan, amesema michezo ina mchango mkubwa katika kuwajengea wanafunzi umoja na ushirikiano, kuwasaidia kufahamiana pamoja na kuimarisha afya zao za kiakili na kimwili.
Naye Afisa Mikopo wa SUZA, Ndugu Abdulkadir Hamid Masoud, ameeleza umuhimu wa wanafunzi kuwa na bima ya afya, akisema huduma hiyo itawasaidia kupata matibabu na msaada wa haraka wanapokabiliwa na changamoto za kiafya wakiwa chuoni. Amewataka wanafunzi kujiandaa kujiunga na mpango huo, akifafanua kuwa taratibu za usajili zinatarajiwa kukamilika hivi karibuni, ambapo kila mwanafunzi atapatiwa namba ya malipo (Control Number) kwa ajili ya kulipia huduma hiyo.
Bonanza hilo limeshirikisha wanafunzi kutoka kampasi mbalimbali za SUZA na kujumuisha michezo tofauti, ikiwemo soka, ambapo timu ya Kampasi ya Kizimbani ilifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuifunga timu ya Kampasi ya Nkrumah kwa mikwaju ya penalti 8–7. Katika mchezo mwingine wa soka, timu ya wanafunzi wanaoendelea na masomo (Continuing Students) kutoka Kampasi ya Tunguu iliibuka na ushindi wa bao moja kwa bila (1–0) dhidi ya timu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza (First Year).
Katika mashindano mengine, Ndugu Hussein Ali Abdalla aliibuka mshindi katika mchezo wa kufukuza kuku, huku Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa SUZA (SUZASO), Ndugu Fatma Miraji Msomi, akishinda mashindano ya kukuna nazi na kula matikiti kwa upande wa wanawake. Michezo mingine iliyofanyika ni kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake pamoja na mashindano ya kula matikiti kwa wanaume.
Bonanza hilo limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Wanafunzi sote tujisajili katika Bima ya Afya ya ZHSF”, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa na kuhamasisha wanafunzi kujiunga na mfuko huo ili waweze kupata huduma za afya kwa urahisi na uhakika zaidi.
