














Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Afrika inahitaji kuwekeza katika tafiti za afya, ubunifu na matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence) ili kupata suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuimarisha utoaji wa huduma za afya barani humo.
Akizungumza kwa niaba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, katika mkutano wa 40 wa Shirikisho la Wanafunzi Madaktari Afrika (FAMSA) ulilofanyika katika ukumbi wa Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC, Maisara Mjini Ugunja, tarehe 5 Novemba 2026.
Amesema maendeleo ya sekta ya afya barani Afrika yanahitaji kizazi cha wataalamu wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa kukabiliana na changamoto za kiafya. Ameeleza kuwa matumizi ya akili unde yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha tafiti za kitabibu, kuboresha uchunguzi na matibabu ya wagonjwa pamoja na kuongeza ufanisi wa huduma za afya.
Aidha amewataka wanafunzi hao kutumia fursa ya mkutano huo kujenga mitandao ya kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuibua mawazo yatakayosaidia kukabiliana na changamoto za afya zinazozikabili jamii za Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara hiyo, Nd. Omar Mwalimu Omar, amesema FAMSA ina jukumu muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya, kuhamasisha uchangiaji wa damu pamoja na kutoa elimu kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, hatua zitakazosaidia kuongeza uelewa wa jamii na kukabiliana na magonjwa hayo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Jamal Jumanne Athumani, amesema ushiriki wa wanafunzi wa SUZA katika mkutano huo umewapa fursa muhimu ya kufahamu kwa undani mazingira halisi ya taaluma ya udaktari, changamoto zake pamoja na mahitaji ya soko la ajira.
Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Nd. Wahida Ali, ameeleza kuwa mkutano huo umejikita katika kuendeleza sekta ya afya barani Afrika kupitia tafiti, ubunifu na matumizi ya akili unde, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote.
