Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA itaendelea kushirikiana na CUBA katika Elimu , Tafiti na Ubunifu

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Jamal Jumanne Athuman, amesema ushirikiano baina ya Cuba na Tanzania umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini, hususan katika mafunzo ya kada za afya.

Prof. Jamal ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuwaaga walimu kutoka nchini Cuba waliokuwa wakifundisha katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kipindi cha miaka mitano kwenye kada mbali mbali za afya.

Amesema katika kipindi chote walichohudumu , walimu hao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufundisha, kuhamisha maarifa na kukuza ujuzi kwa wanafunzi wa kada mbalimbali za afya, hatua iliyosaidia kuimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo.

Prof. Jamal ameongeza kuwa SUZA itaendelea kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani katika sekta ya elimu, kwa lengo la kubadilishana maarifa, uzoefu na teknolojia pamoja na kukuza ubora wa mafunzo na tafiti.

Kwa upande wake, Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, SUZA, Dkt. Salma Abdi Mahmoud ametoa shukrani kwa walimu hao kwa ushirikiano, kujituma na uwajibikaji waliouonesha katika kipindi chote cha miaka mitano, akisema mchango wao umeacha alama muhimu katika maendeleo ya skuli hiyo na kuwajengea wanafunzi msingi imara wa taaluma za afya.

Nae , Mkuu wa Idara ya Patholojia na Biokemia, SUZA, Dkt. Chukwuma James Okafor, amesema chuo kitaendelea kujivunia mchango na uwepo wa walimu hao katika kipindi chote walichohudumu, akieleza kuwa kuondoka kwao nchini hakumaanishi mwisho wa mahusiano hayo, bali SUZA itaendelea kudumisha mawasiliano na kuendeleza ushirikiano nao katika nyanja mbalimbali za kitaaluma.

Wakizungumza mara baada ya sherehe hiyo baadhi ya walimu walioagwa wameeleza kufurahishwa na ushirikiano walioupata kutoka SUZA katika kipindi chote cha miaka mitano.

Hafla hiyo imefanyika katika Mgahawa wa Alannur, Mbweni, Mjini Unguja tarehe 4 Oktoba 2026.