





















Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa, amesema Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimepiga hatua kubwa katika maendeleo ya elimu ya juu, si kwa Zanzibar pekee bali pia katika ukanda wa Afrika, kupitia mchango wake katika kukuza elimu, tafiti na ubunifu.
Akizungumza katika Matembezi ya Mshikamano yaliyoandaliwa na SUZA ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho, yaliyofanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Mhe. Kitwana amesema kuwa katika kipindi cha miaka 25, SUZA imeendelea kupanua wigo wa maendeleo ya kitaaluma na kuongeza fursa za elimu ya juu kwa wananchi kupitia udahili wa wanafunzi katika programu mbalimbali za masomo.
Ameeleza kuwa SUZA imekuwa taasisi muhimu katika kuchangia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akisisitiza kuwa Chuo hicho ni tanuri la kuandaa na kuibua mawazo, maarifa na mipango inayochangia maendeleo ya taifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa viongozi na wafanyakazi wa SUZA, akihimiza kuwepo kwa mazingira ya kazi yasiyo na ubaguzi wa aina yoyote. Amemtaka Makamu Mkuu wa Chuo kuendelea kuimarisha mshikamano huo katika taasisi nzima ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Chuo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kitwana amempongeza Makamu Mkuu wa Chuo kwa namna alivyoanza kutekeleza majukumu yake ya uongozi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano katika kufikia malengo ya maendeleo ya SUZA.
Akizungumzia juhudi za kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu, Mgeni Rasmi alichangia kiasi cha shilingi milioni moja katika mpango wa Goli la Faraja, unaolenga kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika Chuo hicho. Mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuhakikisha wanafunzi hao wanapata fursa na mazingira bora ya kutimiza ndoto zao za kitaaluma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Mohamed Ali Abdalla, ameahidi kuunga mkono mpango wa kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa SUZA, akieleza umuhimu wa wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhakikisha kundi hilo linapata msaada unaostahili.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Said Ali Hamad Vuai, amewashukuru viongozi wa Serikali, viongozi wa Chuo, wafanyakazi, wanafunzi na wananchi walioshiriki katika matembezi hayo, akieleza kuwa shughuli hiyo imelenga kuimarisha mshikamano na ushirikiano baina ya viongozi waliowahi kukitumikia Chuo, viongozi wa sasa pamoja na wafanyakazi wote wa SUZA.
Prof. Vuai pia amezungumzia umuhimu wa kuanzishwa na kuimarishwa kwa Mfuko wa Maendeleo wa Chuo (Endowment Fund), ambao unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kukusanya rasilimali kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya SUZA, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu na ujenzi wa majengo ya kisasa kwa ajili ya Skuli ya Afya.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la SUZA, Dkt. Slim Salum Abdallah, amewahimiza washiriki wa matembezi hayo na jamii kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara, akieleza kuwa mazoezi ni muhimu katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Matembezi hayo ya Mshikamano yalianzia katika Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Mazizini na kuhitimishwa katika Viwanja vya Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja. Yameshirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa SUZA, wafanyakazi, wanafunzi na wadau wengine ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 25 ya Chuo hicho.
Maadhimisho hayo yanaakisi safari ya robo karne ya SUZA katika kutoa elimu ya juu, kuendeleza tafiti na ubunifu pamoja na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Zanzibar na Afrika kwa ujumla.
