Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA YAADHIMISHA MIAKA 90 YA PROF. SALEH IDRIS MUHAMMED KATIKA MATEMBEZI YA MSHIKAMANO YA MIAKA 25 YA CHUO

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeadhimisha miaka 90 ya kuzaliwa kwa Prof. Saleh Idris Muhammed, Makamu Mkuu wa Kwanza wa Chuo hicho, kupitia tukio maalumu la kumpongeza, kukata keki na kumkabidhi zawadi ya siku yake ya kuzaliwa, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wake katika historia na maendeleo ya Chuo.

Tukio hilo limefanyika katika Viwanja vya Maisara, Unguja, sambamba na Matembezi ya Mshikamano yaliyoandaliwa na SUZA ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Katika tukio hilo, Mgeni Rasmi ambae ni Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, alimkabidhi Prof. Saleh Idris Muhammed zawadi maalumu ya siku yake ya kuzaliwa kama ishara ya pongezi na heshima katika kutambua siku hiyo muhimu.

Maadhimisho hayo yameongeza upekee katika sherehe za miaka 25 ya SUZA kwa kuunganisha kumbukumbu ya siku muhimu ya kuzaliwa kwa mmoja wa viongozi wa mwanzo wa Chuo hicho na safari ya robo karne ya taasisi hiyo katika kutoa elimu ya juu na kuchangia maendeleo ya Zanzibar.

Prof. Saleh Idris Muhammed ni miongoni mwa viongozi waliokuwa na nafasi muhimu katika safari ya maendeleo ya SUZA, hususan katika kipindi cha mwanzo cha ujenzi wa taasisi hiyo. Kutambuliwa kwake katika maadhimisho hayo kunaakisi umuhimu wa kuthamini mchango wa viongozi waliotangulia, ambao juhudi na utumishi wao vimekuwa sehemu ya msingi wa maendeleo ya Chuo.

Matembezi hayo ya Mshikamano yalianzia katika Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Mazizini na kuhitimishwa katika Viwanja vya Maisara, yakishirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa Chuo, wafanyakazi, wanafunzi na wadau wengine.

Kupitia maadhimisho hayo, SUZA imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuthamini historia, kutambua mchango wa viongozi wake na kuimarisha mshikamano baina ya viongozi wa zamani na wa sasa pamoja na jumuiya nzima ya Chuo.

Tukio hilo limekuwa sehemu ya kumbukumbu ya miaka 90 ya kuzaliwa kwa Profesa Saleh Idris Muhammed na miaka 25 ya SUZA, likibeba ujumbe wa kuthamini historia, kuheshimu mchango wa waliotangulia na kuendeleza umoja katika safari ya kujenga Chuo chenye mchango mkubwa katika elimu ya juu na maendeleo ya jamii.