Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar Ofisi ya Pemba, kimeendesha mafunzo ya Usalama na Usafi wa Chakula pamoja na Usalama na Maandalizi ya Dharura kwa wamiliki na wahudumu wa migahawa mbalimbali inayotoa huduma za chakula Kisiwani Pemba.
Mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa wa washiriki kuhusu umuhimu wa usalama wa chakula, usafi binafsi, matumizi sahihi ya vifaa vya kinga, njia za kuzuia uchafuzi wa chakula na mbinu bora za uhifadhi wa chakula ili kulinda afya za walaji na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa.
Aidha, washiriki walijifunza namna ya kutambua hatari zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya kazi, kuzuia ajali, kuandaa mipango ya dharura, kutoa huduma ya kwanza kwa waathirika wa ajali pamoja na hatua za kuchukua wakati wa matukio ya dharura kama vile moto au mtu anayekabwa na chakula.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya huduma za chakula
( Local Restaurants) na kutoa fursa kwa washiriki kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kuuliza maswali kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Wamiliki na wahudumu walioshiriki walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo kutokana na maarifa na ujuzi walioupata, wakieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuimarisha viwango vya usalama, usafi na ubora wa huduma katika migahawa yao, sambamba na kuchangia afya bora kwa wananchi na wageni wanaotembelea Kisiwa cha Pemba.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuimarisha viwango vya huduma katika sekta ya utalii na ukarimu kisiwani Pemba kupitia elimu na ujenzi wa uwezo kwa wadau wa sekta hiyo ikiwa ni miongoni mwa juhudi za kuifungua Pemba Kiutaliii.
Mafunzo hayo yamefanyika Pemba na Unguja
