Skip to main content

The State University Of Zanzibar

WAZIRI WA ELIMU AKAGUA MIRADI YA HEET SUZA, ASISITIZA UTEKELEZAJI WA MIKATABA KWA WAKATI

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, amewataka wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya ujenzi inayoendelea katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuhakikisha wanazingatia masharti ya mikataba na kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Mhe. Waziri ametoa kauli hiyo tarehe 2 Julai 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Kilimo na Maabara za Sayansi zinazojengwa kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) katika kampasi ya SUZA, Tunguu.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya elimu ya juu ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia, kufundishia na kufanya tafiti, hivyo ni muhimu kwa wadau wote wanaohusika na utekelezaji wa miradi hiyo kutimiza wajibu wao kwa ufanisi na uwajibikaji.

Akizungumza katika ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Said Ali Hamad Vuai, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya Chuo kupitia Mradi wa HEET.

Prof. Vuai amesisitiza umuhimu wa mshauri elekezi na wakandarasi kutekeleza wajibu wao ipasavyo katika kipindi kilichobaki ili kuhakikisha majengo ya Skuli ya Kilimo na Maabara za Sayansi yanakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa ubora unaotarajiwa.

“Miradi hii ni muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu, tafiti na mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wetu. Tunatarajia kuona kazi zilizobaki zikikamilishwa kwa wakati ili Chuo kiweze kunufaika na uwekezaji huu mkubwa wa Serikali,” amesema Prof. Vuai.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa HEET, Dkt. Haji Ali Haji, amesema mradi huo unatekelezwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, huku SUZA ikinufaika kupitia ukarabati wa maabara za kompyuta, uboreshaji wa mitaala, pamoja na ujenzi wa maabara za kisasa za sayansi na jengo la maabara ya kilimo.

Naye Mshauri Elekezi kutoka kampuni ya Anova, Eng. Eliki Nziku, amesema maendeleo ya ujenzi yamefikia asilimia 80 na miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 28 Julai 2026 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 32.

Ziara hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, uongozi wa SUZA, washauri elekezi na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.