The State University Of Zanzibar

Michezo Yaunganisha SUZA na IIT Madras

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimehimizwa kuendeleza utamaduni wa michezo kwa kuandaa matukio ya michezo angalau mara moja kila semista, hatua inayolenga kuimarisha afya, kuchangamsha akili na kuongeza ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi na wanafunzi.

Wito huo umetolewa na Kaimu Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Abdi Talib Abdalla, wakati akifungua tamasha la SUZA Sports Day lililowakutanisha wafanyakazi wa SUZA na IIT Madras katika viwanja vya Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Mbweni, tarehe 14 Juni 2026

Prof. Abdalla alisema michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga afya bora ya mwili na akili, sambamba na kuimarisha mshikamano na mahusiano mema katika mazingira ya kazi na elimu.

Tamasha hilo lilijumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, ringi mzunguko, mbio za mbatata, kufukuza kuku, kula tikiti na kuonesha vipaji, ambapo washiriki walionesha ari kubwa, ushindani wa kirafiki na mshikamano wa hali ya juu.
Kwa upande wao, wawakilishi wa IIT Madras waliishukuru SUZA kwa ushirikiano na ukarimu walioupata, wakieleza kuwa tukio hilo limeendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili.

Katika mechi ya kirafiki ya mpira wa miguu iliyochezwa kati ya SUZA na IIT Madras, timu zote zilionesha kiwango kizuri cha mchezo na hatimaye kutoka sare ya bila kufungana (0–0), matokeo yaliyoakisi urafiki, mshikamano na heshima iliyotawala katika tamasha hilo.