The State University Of Zanzibar

Ushirikiano wa SUZA na RT waimarisha uwezo wa wanafunzi wa habari

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kupitia Idara ya Mawasiliano na Mafunzo ya Habari, kimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukuza taaluma ya habari baada ya wanafunzi wake kushiriki mafunzo maalumu yaliyotolewa na Taasisi ya Habari ya Kimataifa ya Russia Today (RT) katika Kampasi ya Kilimani.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mafunzo ya Habari wa SUZA, Dkt. Saleh Koshuma, amesema kuwa programu hiyo ni sehemu ya jitihada za chuo za kuwajengea wanafunzi uwezo wa kitaaluma na kuwapa fursa ya kujifunza mbinu za kisasa zinazotumika katika tasnia ya habari duniani.

Dkt. Koshuma amesema ushirikiano kati ya SUZA na RT una mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano ya kielimu kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Urusi, huku ukiwawezesha wanafunzi kupata uzoefu na maarifa kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu katika vyombo vya habari vya kimataifa.

Amefafanua kuwa mafunzo hayo yalijikita katika maeneo mbalimbali ya uandishi wa habari, ikiwemo ukusanyaji wa taarifa, uandishi wa habari, utayarishaji wa maudhui na uwasilishaji wa habari kwa kuzingatia misingi ya taaluma, maadili na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Kwa upande wao, wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na fursa hiyo wakisema imewaongezea maarifa, ujuzi na uelewa mpana kuhusu namna ya kuandaa na kuwasilisha habari kwa weledi, usahihi na ubunifu unaokidhi mahitaji ya hadhira katika mazingira ya sasa ya vyombo vya habari.

Mafunzo hayo ni sehemu ya dhamira ya SUZA ya kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira na kuchangia maendeleo ya sekta ya habari nchini na kimataifa.