The State University Of Zanzibar

SUZA Yaendelea Kukuza Ubora wa Kitaaluma Kupitia SUZASO Awards 2026

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeendelea kuonesha dhamira yake ya kuendeleza ubora wa kitaaluma, ubunifu na uongozi wa wanafunzi kupitia hafla ya utoaji wa tuzo za SUZASO Awards 2026, ambapo wanafunzi bora katika nyanja mbalimbali walitunukiwa tuzo kwa kutambua juhudi, vipaji na mafanikio yao ya kitaaluma.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika tarehe 28 Juni 2026 katika Ukumbi wa Michenzani Mall, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema mashindano ya kitaaluma ni nyenzo muhimu ya kuimarisha utamaduni wa kujifunza, kukuza ubunifu na ushindani chanya miongoni mwa wanafunzi.

Amesema tuzo hizo zinasaidia kuibua vipaji, kuthamini juhudi za wanafunzi na kuhamasisha ubora katika sekta ya elimu, huku akiipongeza SUZA na Serikali ya Wanafunzi (SUZASO) kwa kuanzisha jukwaa hilo muhimu linalochochea maendeleo ya wanafunzi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo, Prof. Said Ali Hamad Vuai, amesema chuo kitaendelea kuimarisha mazingira yanayowezesha wanafunzi kufikia viwango vya juu vya umahiri, ubunifu na ushindani katika soko la ajira.

Hafla ya SUZASO Awards 2026 imefanyika kwa mara ya nne tangu kuanzishwa kwake, ambapo jumla ya tuzo 23 zilitolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali.