The State University Of Zanzibar

Prof. Hikmany: SUZA itaendelea kuunga mkono elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Hamed Rashid Hikmany amaesema SUZA itaendelea kuunga mkono na kuimarisha elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata fursa sawa za elimu na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Akizungumza na wanafunzi, walimu na wadau wa taasisi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mradi wa Breaking Education Barriers: Inclusion, Rehabilitation, and Technology (BERT) amelezea kuwa SUZA itaendelea kudumisha mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kielimu.

Prof. Hikamany ametoa wito kwa waajiri kutoa fursa za ajira kwa watu wenye ulemavu kwa kuzingatia uwezo, ujuzi na weledi wao badala ya kuangalia changamoto zao za kimwili. Aidha, amezitaka taasisi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu kuendelea kushirikiana na vyuo vikuu katika kutoa ushauri na miongozo itakayosaidia kuimarisha huduma na mazingira jumuishi kwa kundi hilo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Kiongozi Mkuu wa mradi huo katika Chuo Kikuu cha Taifa ambaye pia ni Mkuu wa Skuli ya Elimu cha Zanzibar SUZA, amabe pia ni Mkuu wa Skuli ya Elimu , Dkt. Said Khamis Juma amesema lengo kuu la programu hiyo ni kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwapatia uelewa wa kina kuhusu taratibu za ajira, fursa za kujiajiri na kuajiriwa, pamoja na kuwajengea uwezo wa kujiandaa kwa ushindani wa soko la ajira.

Amesema mafunzo hayo yanajumuisha mbinu za kuandika wasifu wa kazi (CV) unaokidhi viwango vya kitaaluma, taratibu za kuomba ajira, pamoja na namna ya kufanya vizuri katika usaili wa kazi. Aidha, amewasisitiza wanafunzi kutumia vyema kipindi chao cha masomo chuoni kwa kujifunza maarifa na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Sera wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Ndg. Abushiri Said Khatibu, amesema malengo ya baraza hilo ni kuhakikisha ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali za maendeleo, kukuza uelewa wa jamii kuhusu haki zao na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu, ajira na huduma nyingine za kijamii.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa programu hiyo itawasaidia kuongeza uelewa kuhusu maandalizi ya kuingia katika soko la ajira, kujiamini katika kuomba kazi na kutambua fursa mbalimbali za kujiajiri, huku wakiiomba SUZA na wadau wengine kuendelea kuandaa mafunzo kama hayo kwa manufaa ya wanafunzi na wahitimu.

Mradi wa BERT (2023–2026), unaofadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, unalenga kuimarisha elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kupitia teknolojia, urekebishaji na ushirikiano wa kimataifa.