


Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA Prof Abdi Talib Abdlalla amekutana na wanafunzi kumi na watano (15) pamoja na wafanyakazi wanne (5) kwa lengo kwa kuwaaga kabla ya safari yao ya kwenda nchini Romania kushiriki katika programu ya kubadilishana uzoefu ya wiki mbili inayofadhiliwa na European Union kupitia programu ya Erasmus Programme.
Akiwapa nasaha katika Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu SUZA Tunguu wilaya ya Kati Unguja, Prof Abdi amesema kuwa washiriki hao wanatakiwa kujikita zaidi na malengo yaliyowapeleka ili kufikia kusudio la mradi huo.
Aidha amewaasa kufuata sheria za nchi wakati wote wanapokuwa nchini humo ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.
Sambamba na hayo awetaka kujifunza mambo mbalimbali ya kitaaluma ambayo yatasaidia kuengeza ujuzi mpya kupitia nidhamu, ubunifu, na ushirikiano wa kimataifa.
Nae kiongozi wa program hiyo kwa upande wa SUZA Dkt Abubakar Diwani amewaasa kujenga tabia ya kuwa wavumilivu, kustahamili changamoto mbalimbali, na kuweza kutambua njia bora za kutatua changamoto zinawakabili wakiwa ugenini.
Programu ya kubadilishana uzoefu nchi Romania, itawakutanisha washiriki kutoka vyuo vikuu 15 vya Afrika, Asia na Ulaya katika Blended Workshop inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kubadilishana maarifa, na kujenga uwezo katika maeneo ya Utalii, ICT, na Mazingira.