The State University Of Zanzibar

SUZA YASHIRIKI KONGAMANO LA WANAFUNZI WA MAABARA TANZANIA

Wanafunzi wa kada ya Maabara wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar wameshiriki Kongamano la Kumi na Moja (11) la Jumuiya ya Wanafunzi wa Maabara Tanzania (TAMELASA). Kongamano hilo limefanyika tarehe 16/05/2026 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam.

Akihutubia Kongamano hilo Mgeni Rasmi, Mhe. Wanu Hafidhi Ameir, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ametoa maagizo kwa Taasisi zinazosimamia Taaluma za Afya kwa kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEVET) kuweka viwango vya elimu vinavyofanana Kitaifa ili kuweza kutoa wahitimu wenye umahiri ulio sawa. Aidha alitumia jukwaa hilo kupongeza juhudi za viongozi hao na kuwahimiza wanafunzi kutumia fursa za majukwaa kama haya kujifunza, kujenga majukwaa ya mitandao, na kuwa wabunifu katika taaluma ya maabara.

Akiwasilisha mada katika Kongamano hilo Ndg. Saleh Shein Makame mkufunzi kutoka wa SUZA ambaye pia ni Mlezi Jumuiya ya Wanafunzi wa Maabara TAMELASA Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, amebainisha umuhimu wa kuwajenga wanafunzi kielimu na kijamii ili waweze kupata uzoefu wa kutosha katika Taaluma ya Maabara.

Shein aliwasisitiza wanafunzi hao namna elimu ya kijamii inavyosaidia kuwa na uwezo wa kuwasiliana, kushirikiana, na kujitangaza katika fani ya maabara, siyo kitaaluma tu bali na kimaadili na kiuwezo wa kutatua changamoto.