





Mwenyekiti wa Kigoda cha Sheikh Abeid Amani Karume katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Eginald Mihanjo, amesema falsafa na urithi wa waasisi wa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheikh Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni nguzo muhimu katika kulijenga Taifa na kulifikisha kwenye hatua za maendeleo. Ameeleza hayo katika mdahalo uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinatul Bahar, Mjini Unguja.
Akizungumza katika mdahalo wa wazi ulioandaliwa na SUZA wenye mada isemayo, “Maisha na urithi wa falsafa za Sheikh Abeid Amani Karume na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni chachu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania”, Prof. Mihanjo alisema viongozi hao waliweka msingi imara wa maendeleo kupitia misingi ya umoja, usawa na kujitegemea.
Aidha, Prof. Mihanjo ameongeza kwamba waasisi hao walihakikisha Muungano unakuwa chombo cha ukombozi wa maendeleo, ukiwa na dhima ya kuchochea ustawi wa wananchi na kutokomeza athari za mifumo kandamizi ikiwemo urithi wa utumwa.
Katika hatua nyingine, Prof. Mihanjo aliziomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kuwekeza zaidi katika kuwaandaa vijana kwa kuwajengea maadili ya uongozi na kuwalea katika misingi bora, ili kuepuka matumizi mabaya ya madaraka wanapopewa nafasi za uongozi na hivyo kuendeleza falsafa za waasisi wa Taifa.
Akichangia mada hiyo, Prof. Haji Semboja amesema hayati Abeid Amani Karume alikuwa kiongozi mwenye uzalendo, aliyejitoa kwa maendeleo ya jamii, na kuwataka vijana kuenzi misingi hiyo ili kuendeleza ukuaji wa uchumi.
Naye Prof. Mohammed Hafidh amesema viongozi hao waliimarisha mahusiano ya kimkakati na mataifa mengine ya Afrika, hatua iliyochangia kupanua ushirikiano wa maendeleo katika bara hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi Jamii SUZA, Dkt. Saada Omar Wahaab, alisisitiza umuhimu wa kuwajengea vijana uzalendo na kuwafundisha historia ya Taifa ili kulinda na kuendeleza urithi wa waasisi wetu.
Hata hivyo Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Bwana Khamis Mbeto Khamis, amesema misingi ya umoja na mshikamano iliyowekwa na viongozi hao inapaswa kuendelezwa, huku akihimiza maridhiano miongoni mwa viongozi kwa ustawi wa Taifa.
Kigoda cha Sheikh Abeid Amani Karume katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kilizinduliwa rasmi mwaka 2024 na Rais wa awamu ya nane wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na hadi sasa kimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuendeleza fikra za waasisi wa Taifa letu.