Na Mwandishi wetu, SUZA.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Abdi T. Abdalla, amefungua rasmi mafunzo ya wakuu wapya wa idara kutoka skuli mbalimbali za chuo hicho, yanayolenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji na kiuongozi.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, amewataka wakuu hao wa idara kufanya kazi kwa ufanisi, wakizingatia sera za chuo na miongozo ya taifa, ili kuhakikisha wanazalisha wasomi bora wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za jamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuhimiza uanzishwaji wa mifumo madhubuti ya usimamizi wa kazi za kila siku kwa kushirikiana na wanataaluma wengine ndani ya chuo.
Katika kuendana na hadhi na ukuaji wa chuo, amewahimiza wakuu hao kufikiria na kubuni fursa mpya za kitaaluma kwa kuongeza kozi katika ngazi mbalimbali, ikiwemo shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu.
Sambamba na hilo, amewataka kuwekeza zaidi katika tafiti zitakazochochea ubunifu na kuleta fursa mpya za mapato ya ndani kupitia idara zao.
Pia amesisitiza uzingatiaji wa maadili ya kazi na nidhamu ya utendaji, akibainisha kuwa hayo ni msingi muhimu wa kuimarisha ufanisi wa chuo kwa ujumla.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Skuli ya Kompyuta na Masomo ya Habari ya SUZA, na yanatarajiwa kuendelea kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo tarehe 27-04-2026.
