



Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) imekikabidhi rasmi Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar (ZIToD) kwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar (WUMK), hatua inayolenga kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Kaimu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga, amesema uamuzi wa kukiondoa chuo hicho kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ni sahihi na utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa mafunzo ya utalii.
Amesema lengo kuu ni kuimarisha mafunzo ya vitendo ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la kimataifa.
“Tutahakikisha Chuo hiki kinapiga hatua zaidi kwa kuongeza ubora wa mafunzo na huduma zake,” alisema Soraga.
Ameongeza kuwa Chuo hicho kitaanza kutoa huduma za hoteli kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uzoefu wa vitendo, pamoja na kuongeza mchango wake katika pato la taifa.
Aidha, amesema wizara hiyo inapanga kuingia makubaliano na Taasisi ya Utalii ya Oman (Oman National Hospitality Institute) ili kuwawezesha wahitimu kupata vyeti vitakavyowapa nafasi ya ajira ndani na nje ya Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohammed Musa, amewataka watendaji wa chuo hicho kuhakikisha wanakiendeleza ili kiendane na kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii duniani.
Amesema sekta ya utalii ni mhimili mkubwa wa uchumi wa Zanzibar, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa ikazingatia viwango vinavyokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Nae Prof.Abdi Kaimu i Makamu Mkuu wa Chuo cha taifa cha Zanzibar ( SUZA) amesema SUZA itaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbali mbali ya kitaaluma pamoja na ushirikiano ili ZIToD iendelee kukua zaidi na kuleta mabadiliko makubwa ya sekta ya utalii Zanzibar.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika ukumbi wa ZIToD na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa sekta ya utalii pamoja na wahadhiri na kutoka vyuo mbalimbali.