The State University Of Zanzibar

Mradi wa RES4CLIMA kuokoa upotevu wa mazao Pemba

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) anayeshughulikia masuala ya Fedha, Mipango na Utawala, Prof. Salum Seif Salum, amekutana na ujumbe wa mradi wa RES4CLIMA wenye lengo la kuokoa upotevu wa mazao ya matunda na mbogamboga kwa wakulima wadogo kisiwani Pemba.

Ujumbe huo ulijumuisha wataalamu sita kutoka vyuo vikuu vya Milano na Brescia vya nchini Italia ambao uliwasilisha mpango kazi wa kuandaa program za mafunzo, kuundwa kwa kamati ya uratibu ya mipango, pamoja na utekelezaji wa programu zilizoandaliwa kwa vitendo ili kuongeza mavuno ya mazao ya matunda na mboga mboga.

Prof. Salum aliuambia ujumbe huo kuwa SUZA itatoa kila aina ya ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unafikia malengo yaliyokusudiwa kwa wakati. Sambamba na hayo aliwataka wataalamu hao kusaidia kutoa mafunzo kwa watendaji wa maabara za sayansi ili kupata watendaji watakaotumia vyema vifaa
vya kisasa vilivyopo.

Katika hatua nyengine, ujumbe huo ulitembelea maabara za Sayansi zilizopo Kampasi ya Tunguu pamoja na skuli ya Kilimo Kizimbani.

Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 23/02/2026 katika ofisi za makao makuu ya SUZA Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja yaliwashirikisha viongozi na maofisa kutoka skuli na Idara za SUZA.

Ushirikiano kati ya SUZA na vyuo vikuu vya Milano na Brescia unajikita katika utafiti wa kisayansi na matumizi ya teknolojia rafiki wa mazingira ili kupunguza upotevu wa mazao (post-harvest losses), pia wanajihusisha na miradi ya kubadilisha mabaki ya matunda (fruit waste) kuwa nishati au mbolea (circular
economy).

Res4Clima ni mradi wa maendeleo unaolenga kuimarisha ustahamilivu wa jamii za vijijini Tanzania dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, mradi huu hushughulikia masuala ya maji, kilimo, na usimamizi wa ardhi ili kuwasaidia watu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.