Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA YAWATAKA WANAFUNZI WAPYA KUTUMIA VYEMA RASILIMALI ZA CHUO KWA MAFANIKIO YA KITAALUMA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Said Ali Hamad Vuai, amewataka wanafunzi wapya waliojiunga na Chuo hicho kwa mwaka wa masomo 2026/2027 kutumia ipasavyo rasilimali zinazopatikana chuoni ili kuimarisha ufaulu wao wa kitaaluma, ujifunzaji na utafiti.

Prof. Vuai ameyasema hayo wakati wa Wiki ya Ukaribisho kwa Wanafunzi Wapya wa SUZA, iliyofanyika katika Makao Makuu ya Chuo hicho, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, akieleza kuwa Chuo kimeendelea kupiga hatua katika kuboresha miundombinu na kuweka vifaa vya kisasa vinavyowezesha ufundishaji, ujifunzaji na utafiti.

Alieleza kuwa rasilimali hizo zinajumuisha maabara zenye vifaa vya kisasa, maeneo ya kujifunzia, maktaba na huduma mbalimbali zinazowawezesha wanafunzi kutimiza malengo yao ya kitaaluma.

Aidha, Prof. Vuai alisema SUZA itaendelea kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Kampasi Jumuishi kwa kuimarisha matumizi bora ya ardhi na miundombinu iliyopo, ikiwemo kujenga majengo yenye ghorofa nyingi pale itakapohitajika ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya Chuo.

“Tutafuata mpango mkuu wa kampasi jumuishi, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo yenye ghorofa nyingi pale itakapohitajika ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nafasi,” alisema Prof. Vuai.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdalla, aliwahimiza wanafunzi hao kuwa na nidhamu, kutumia muda wao vizuri na kuzingatia taratibu na kanuni za Chuo ili kufikia malengo yao ya kitaaluma.

Prof. Abdalla alisisitiza umuhimu wa kuhudhuria vipindi vya masomo kwa kuzingatia kiwango cha chini cha mahudhurio kinachotakiwa, ambacho ni asilimia 75, akieleza kuwa mahudhurio ni miongoni mwa mambo muhimu yanayochangia uelewa wa masomo na kutimiza masharti ya kustahili kufanya mitihani ya mwisho.

“Mafanikio chuoni hayaji kwa bahati, bali yanajengwa kwa juhudi na bidii. Hivyo, tusome kwa bidii,” alisisitiza Prof. Abdalla.

Akizungumzia matumizi ya teknolojia katika elimu, Prof. Abdalla aliwataka wanafunzi kutumia teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence—AI) kwa uwajibikaji, akionya dhidi ya matumizi yanayoweza kusababisha udanganyifu wa kitaaluma na kudhoofisha uwezo wao binafsi wa kujifunza.

“AI iwe msaidizi wako, si mbadala wako. Itumie kujifunza vizuri, si kuibia,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa wanafunzi wanapaswa kutumia kikamilifu rasilimali za Chuo, zikiwemo vyumba vya madarasa, maktaba, maabara na huduma za intaneti zinazopatikana katika kampasi mbalimbali. Aidha, alieleza kuwa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu wametengewa maeneo maalumu kwa ajili ya kujisomea, kufanya mijadala ya kitaaluma na kutekeleza shughuli za utafiti.

Vilevile, wanafunzi walihimizwa kutumia majukwaa ya Chuo kujadili changamoto zinazowakabili, kubadilishana mawazo kwa kuheshimiana na kuthamini tofauti za mitazamo. Msisitizo huo ulilenga kujenga mazingira ya kitaaluma yanayohimiza fikra huru, mijadala yenye tija na ushirikiano miongoni mwa wanafunzi.

Kwa mujibu wa takwimu za udahili kwa mwaka wa masomo 2026/2027, SUZA ilipokea takribani maombi 8,200, ambapo waombaji 4,524, sawa na takribani asilimia 55 ya maombi yaliyopokelewa, walipata nafasi ya kujiunga na Chuo hicho.

Kati ya wanafunzi waliodahiliwa, wanawake ni 2,680, sawa na takribani asilimia 59 ya wanafunzi wote waliopata nafasi za udahili.

Ujumbe wa viongozi wa Chuo kwa wanafunzi wapya unaweka msisitizo katika matumizi bora ya rasilimali za SUZA, nidhamu, uwajibikaji na kujituma katika masomo, mambo yanayotarajiwa kuwasaidia wanafunzi hao kufikia malengo yao na kuchangia maendeleo ya Chuo na jamii kwa ujumla.