Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA YAPOKEA MAJENGO YA MAABARA ZA SAYANSI NA SKULI YA KILIMO YENYE THAMANI YA BILIONI 32 ZA KITANZANIA

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimepokea rasmi majengo mawili ya kisasa ya maabara za sayansi na Skuli ya Kilimo katika Makao Makuu ya Chuo, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, kupitia hafla ya makabidhiano ya kazi za ujenzi iliyofanyika tarehe 20 Oktoba 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET).

Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu – Utawala wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ndugu Amos John Henock, amesema kuwa miundombinu hiyo itachangia kuimarisha utafiti, matumizi ya teknolojia na mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi, sambamba na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Amesema uwepo wa maabara na vifaa vinavyokidhi mahitaji ya kitaaluma utawapa wanafunzi fursa pana zaidi za kujifunza kwa vitendo, kufanya tafiti na kukuza ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maendeleo ya jamii.

Aidha, ametoa pongezi na shukrani kwa uongozi wa SUZA, Baraza la Chuo, mkandarasi Mohammed Builders Ltd. pamoja na mshauri elekezi Arques Africa kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo. Amemtaka mkandarasi kuendelea kuwa karibu na Chuo katika kipindi cha mpito ili kushughulikia changamoto zozote zitakazojitokeza katika matumizi ya majengo hayo.

Amewahimiza wahadhiri, wanafunzi na watumiaji wengine wa miundombinu hiyo kuitunza na kuitumia kwa ufanisi ili iweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa katika ufundishaji, utafiti na ubunifu. Pia ametoa wito kwa Mohammed Builders Ltd. kuangalia fursa za kuwekeza katika ujenzi wa hosteli mbili kubwa za kisasa ndani ya SUZA ili kuunga mkono mahitaji ya makazi yanayotokana na ukuaji wa Chuo.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Prof. Said Ali Hamad Vuai, amesema kukamilika kwa majengo hayo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, kupanua uwezo wa udahili na kuimarisha programu mbalimbali za kitaaluma zinazotolewa na Chuo.

Amesema miundombinu hiyo imekuja wakati muhimu ambapo SUZA inaendelea kuboresha programu zake na kujenga mazingira yanayowawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa ya kitaaluma na soko la ajira.

Prof. Vuai ameeleza kuwa jengo la maabara za sayansi lina maabara 20, huku jengo la Skuli ya Kilimo likiwa na maabara sita, hivyo kufanya jumla ya maabara katika majengo hayo mawili kufikia 26. Amesema maabara hizo zitasaidia wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo na kuwezesha utekelezaji wa mitaala inayolenga kuongeza umahiri na uwezo wa wahitimu katika fani zao.

Amebainisha kuwa SUZA inaendelea kutekeleza kaulimbiu yake ya “Train in Zanzibar, Ready for the World”, inayolenga kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na ujuzi wakiwa Zanzibar, lakini wanakuwa na uwezo wa kufanya kazi na kushindana katika mazingira ya kitaifa na kimataifa.

Aidha, Prof. Vuai ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya elimu ya juu, pamoja na mkandarasi Mohammed Builders Ltd. na mshauri elekezi Arques Africa kwa mchango wao katika kukamilisha mradi huo. Ameipongeza kampuni ya Mohammed Builders Ltd. kwa hatua za ziada ilizochukua, ikiwemo kupaka rangi upya majengo yote mawili na jengo la Utawala, pamoja na kujenga msikiti ndani ya Chuo unaotarajiwa kuhudumia waumini zaidi ya 300.

Amesema kupokea majengo hayo ni hatua inayokifanya Chuo kuanza ukurasa mpya wa maendeleo, hasa katika kipindi ambacho SUZA inaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Ameeleza kuwa miundombinu hiyo ni msingi muhimu wa kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kupanga hatua za maendeleo kwa miaka 25 ijayo.

Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mradi huo, mwakilishi wa mshauri elekezi Arques Africa ameeleza kuwa ujenzi huo ni sehemu ya mpango mkakati unaoratibiwa na kutekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya programu ya HEET. Programu hiyo inalenga kuboresha ubora wa elimu ya juu na miundombinu ya vyuo vikuu nchini.

Amefafanua kuwa jengo la maabara za sayansi limebuniwa kuwa na nafasi mbalimbali za kufundishia, kufanya utafiti na kusaidia shughuli za kitaaluma. Jengo hilo lina kumbi 11 za mihadhara, vyumba sita vya semina, ofisi za watumishi zitakazotumiwa na watumishi 107, maktaba yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 205 na vyumba viwili vya mikutano.

Katika upande wa maabara, jengo hilo lina maabara tano za Kemia, tano za Fizikia na tano za Biolojia, pamoja na maabara moja ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), maabara moja ya Remote Sensing, maabara moja ya Mawasiliano, maabara moja ya Multimedia na maabara moja ya GeoICT. Miundombinu hiyo inalenga kuimarisha mafunzo ya vitendo na shughuli za utafiti katika fani mbalimbali za sayansi na teknolojia.

Kwa upande wa jengo la Skuli ya Kilimo, mshauri elekezi ameeleza kuwa lina maabara tatu za kilimo na maabara tatu za mifugo au wanyama, ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 250, ofisi za watumishi 20, maktaba yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 100 na ukumbi wa mikutano unaoweza kuchukua watu 75. Pia, jengo hilo lina vyumba viwili vya kompyuta, kila kimoja kikiwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 50.

Amesema majengo hayo yameandaliwa ili kuimarisha ufundishaji, utafiti na mafunzo ya vitendo, hususan katika sayansi, kilimo na teknolojia, kwa kutoa mazingira bora yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi na watumishi wa Chuo.

Nae Mohammed Builders Ltd., ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kuweka mazingira bora ya maendeleo ya miundombinu na utekelezaji wa miradi inayowanufaisha wananchi.

Pia ameishukuru timu ya SUZA iliyosimamia mradi huo hadi kukamilika kwake, mshauri elekezi Arques Africa na timu nzima ya Mohammed Builders Ltd., wakiwemo wahandisi, madereva, vibarua na wafanyakazi wengine walioshiriki katika kazi za ujenzi.

Ameeleza kuwa pamoja na kazi za ujenzi wa majengo hayo, kampuni imechangia katika kuboresha mandhari ya Chuo kwa kupaka rangi upya majengo yote mawili na jengo la Utawala, na kujenga msikiti wenye uwezo wa kuhudumia waumini zaidi ya 300.

Mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 32 za Kitanzania ulianza tarehe 4 Desemba 2024 na kukamilika tarehe 30 Septemba 2026. Utekelezaji wake ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu na kuongeza uwezo wa SUZA katika kutoa elimu yenye ubora, kufanya utafiti na kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla