












Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Said Ali Hamad Vuai, amewataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii nchini kuongeza bidii na uadilifu katika utendaji wao, kuifahamu vyema jamii wanayoihudumia na kujiendeleza kitaaluma ili kuboresha afya za wananchi.
Prof. Vuai ametoa wito huo wakati wa mahafali ya pili ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs), yaliyofanyika katika Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Mbweni, Zanzibar, tarehe 17 Oktoba 2026.
Amesema wahudumu hao wana jukumu muhimu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, ili kuwajengea uelewa wa namna ya kujikinga na magonjwa hayo na kuchangia kuboresha afya katika jamii.
Aidha, Prof. Vuai amemshukuru Rais wa Zanzibar kwa kuimarisha sekta ya afya kupitia uwekezaji katika miundombinu, ikiwemo vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mkoa na hospitali za rufaa, pamoja na kutambua umuhimu wa huduma za afya ngazi ya jamii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Dkt. Chukwuma James Okafor, amewapongeza wahitimu hao kwa kufikia malengo yao, huku akiwataka kuzingatia maarifa na maadili ya taaluma yao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Mratibu wa kada hiyo, Dkt. Ali Idarous Adnan, amesema Wizara ya Afya ina mpango wa kuwafikia wananchi wote, mijini na vijijini, kupitia huduma za afya ngazi ya jamii. Hivyo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wahudumu hao wanapowatembelea majumbani mwao.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, Ndg. Abdalla Simai Dora, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha mafunzo hayo, ambayo yamewapatia taaluma na ujuzi wa kuwahudumia wananchi.
Jumla ya wahitimu 97 wamehitimu mafunzo hayo yaliyodumu kwa miezi sita. Mafunzo hayo yalihusisha miezi mitatu ya nadharia darasani na miezi mitatu ya mafunzo ya vitendo katika jamii.
Kupitia mafunzo hayo, wahitimu wamepata ujuzi katika maeneo mbalimbali ya afya, yakiwemo upimaji wa shinikizo la damu, uchunguzi wa VVU na kisukari, pamoja na malaria.
