Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA YAFANYA DUA YA KUWAOMBEA NA KUWAENZI WAFANYAKAZI WALIOTANGULIA MBELE YA HAKI

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Said Ali Hamad Vuai, amesema wafanyakazi wa Chuo hicho waliotangulia mbele ya haki wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taasisi hiyo na sekta ya elimu nchini, hivyo ni muhimu kuendelea kuwaenzi na kukumbuka utumishi wao.

Prof. Vuai ameyasema hayo wakati wa dua maalumu ya kuwaombea wafanyakazi wa SUZA waliofariki dunia, iliyofanyika tarehe 16 Oktoba 2026 katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema wafanyakazi hao walishiriki kwa nafasi na uwezo wao katika safari ya maendeleo ya Chuo, hivyo dua hiyo ni sehemu ya kuwakumbuka, kuwaenzi na kumuomba Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na kuwarehemu.

Aidha, Prof. Vuai amewakumbusha washiriki umuhimu wa kutambua kuwa maisha ya mwanadamu yana mwisho, akisisitiza haja ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kufanya matendo mema na kujiandaa kwa maisha ya Akhera.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la SUZA, Prof. Hamed Rashid Hikmany, amesema dua hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuendeleza mshikamano na kuimarisha juhudi za maendeleo ya Chuo ili kiweze kutimiza malengo yaliyowekwa na waasisi wake.

Prof. Hikmany amesisitiza pia umuhimu wa kuliombea taifa amani na utulivu, huku akimuomba Mwenyezi Mungu alinde nchi dhidi ya majanga mbalimbali yanayoweza kuathiri usalama na ustawi wa wananchi.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Jamal Jumanne Athuman, amewashukuru wote walioshiriki katika dua hiyo na kuhimiza wanajumuiya ya SUZA kuendelea kushiriki katika shughuli za Chuo zinazolenga kuimarisha umoja, mshikamano na mahusiano mema miongoni mwa watumishi.

Amesema ushiriki katika shughuli za pamoja ni muhimu katika kuendeleza utamaduni wa kuthaminiana na kuimarisha jumuiya ya Chuo, huku wakiendelea kukumbuka mchango wa watumishi waliotangulia mbele ya haki.

Dua hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambayo pamoja na kuadhimisha mafanikio na hatua za maendeleo zilizofikiwa, yanatoa fursa ya kuwakumbuka na kuwaenzi watu waliochangia katika safari ya ukuaji wa Chuo hicho.

Kupitia dua hiyo, SUZA imeendeleza utamaduni wa kuwaombea marehemu na kuthamini mchango wa wafanyakazi wake katika kujenga na kuendeleza taasisi hiyo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.