Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeanza rasmi kampeni ya kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu masuala ya kijinsia, huku Timu ya Dawati la Jinsia ikizindua ziara maalum inayolenga wanafunzi, wanataaluma na watumishi wa chuo .
Ziara hiyo imeanza katika Skuli ya Kilimo Kizimbani, ambapo timu hiyo ilikutana na wanafunzi na kuwapatia elimu kuhusu kanuni, sheria na miongozo ya chuo wanapokuwa katika masomo yao. Aidha, wanafunzi walikumbushwa kuhusu athari na adhabu zinazotokana na makosa ya udhalilishaji wa kijinsia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha nidhamu na mazingira salama ya kujifunzia.
Mbali na wanafunzi, timu hiyo pia ilifanya kikao na watumishi wa skuli hiyo, ambapo walipewa nasaha na kukumbushwa wajibu wao wa kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi na kuepuka vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyoweza kusababisha migogoro isiyo ya lazima.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mmoja wa wajumbe wa timu alisisitiza umuhimu wa kila mwanachuo kufahamu na kuzingatia miongozo iliyowekwa, akibainisha kuwa elimu hiyo inalenga kujenga jamii ya chuo yenye usawa, heshima na uwajibikaji.
Ziara ya Dawati la Jinsia SUZA inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine ya chuo, ambapo timu hiyo itatembelea Skuli ya Kompyuta, Mawasiliano na Mafunzo ya Habari iliyopo Kampasi ya Kilimani siku ya Alhamisi, Aprili 30, 2026, kuendeleza juhudi za kutoa elimu na kuimarisha uelewa kuhusu masuala ya kijinsia chuoni humo.