Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimepokea ziara ya wanafunzi kutoka Al-Uhda and Madrasa ya Kisauni Zanzibar, waliotembelea Kampasi ya Tunguu kwa lengo la kujifunza kwa vitendo katika nyanja za teknolojia na mawasiliano.
Katika ziara hiyo, wanafunzi hao walipata fursa ya kujifunza na kushuhudia kwa karibu shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Skuli ya Kompyuta na Masomo ya Habari ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kisasa ya TEHAMA, programu za kompyuta, pamoja na masuala ya mawasiliano ya kidijitali.
Ziara hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa masomo wanayoyasoma darasani kwa kuyaona katika mazingira halisi ya utekelezaji, pamoja na kuwahamasisha kuchagua taaluma zinazohusiana na teknolojia na ubunifu katika elimu ya juu.
Uongozi wa SUZA umepongeza jitihada za shule hiyo kwa kuwaandalia wanafunzi fursa ya kujifunza nje ya darasa, na kusisitiza umuhimu wa ziara za kielimu katika kukuza maarifa na vipaji vya wanafunzi.
SUZA inaendelea kufungua milango kwa jamii ili kuhamasisha elimu ya vitendo na kuandaa kizazi chenye ujuzi na ubunifu.