The State University Of Zanzibar

USHIRIKIANO WA SUZA NA KAMISHENI YA KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI KUWAJENGEA UWEZO WAHITIMU.

Kwa niaba ya Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo , Maafisa wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wamefanya mazungumzo na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki katika ofisi za taasisi hiyo, zilizopo eneo la Maisara, Mjini Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma.

Katika kikao hicho, SUZA imekubali rasmi ombi na fursa iliyowasilishwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ya kufanya kazi kwa pamoja katika kuwajengea uwezo wahitimu wa chuo hicho. Kupitia ushirikiano huo, vijana waliomaliza masomo yao SUZA watanufaika na programu maalum ya mafunzo ya vitendo yatakayodumu kwa kipindi kisichopungua miezi sita.

Mafunzo hayo yanalenga kuwaandaa wahitimu hao kwa ajira za kimataifa na kikanda, kwa kuwapatia ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa.

Kwa mwaka 2026, wahitimu watapata fursa ya kujengewa uwezo katika fani mbalimbali zikiwemo: Fedha, Uhasibu, Uchumi, Biashara, Mipango na Bajeti; Uongozi wa Biashara; Ununuzi, Mnyororo wa Ugavi na Lojistiki; Teknolojia ya Habari ikijumuisha Sayansi ya Kompyuta, Usalama wa Kimtandao na Upangaji Programu; Sayansi ya Taarifa (Data Science); Rasilimali Watu; Mawasiliano ya Jamii na Uandishi wa Habari; Usimamizi wa Ofisi na Ukatibu Muhtasi; pamoja na Sayansi ya Maktaba, Taarifa na Usajili, na Utawala na Uendeshaji.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza ushindani wa wahitimu wa SUZA katika soko la ajira na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya rasilimali watu yenye ujuzi stahiki ndani na nje ya nchi.

SUZA inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kutoa elimu bora inayozingatia mahitaji ya maendeleo ya jamii na uchumi wa kisasa.