

Kaimu Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA Prof Abdi Talib Abdlalla amefanya mazungumzo na ujumbe wa taasisi ya MashUbora ili kushirikiana katika kuimarisha utafiti wa kimatibabu kwa kanda ya Afrika Mashariki.
Akizungumza na ujumbe huo ulioongozwa na Ndg. Sehlomola Mashatole ambaye ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo na Dkt. Salma Abdi Mahmoud Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za tiba SUZA ambaye pia ni Mkurugenzi wa MashUbora kwa kanda ya Afrika Mashariki.
Prof. Abdi ameeleza taasisi hiyo kuwa SUZA imeridhia uwepo wa mashirikiano na taasisi hiyo ili kuimarisha tafiti sambamba na wafanyakazi kupata mafunzo ya kuimarisha tafiti za kimatibabu jambo ambalo litasaidia kuzalisha wataalamu wa sekta ya afya nchini.
Akiitambulisha taasisi hiyo Bwa. Mashatole ameeleza kuwa taasisi hiyo imedhamiria kuweka Visiwa vya Zanzibar kuwa eneo kuu la Afrika Mashariki kwa ubora wa utafiti wa kimatibabu.
Aidha Taasisi hiyo imejitolea kufanya kazi pamoja na serikali, vituo vya huduma za afya, na wadau wa sekta wa afya.
Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 9 April katika Ukumbi wa Mikutano Makao Makuu Tunguu Zanzibar.