The State University Of Zanzibar

Ujumbe wa taasisi ya MashUbora umekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar

Ujumbe wa taasisi ya MashUbora umekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji Ofisini kwake Mnazi Mmoja kwa lengo la kuanzisha ushirikiano na Wizara hiyo.

Akitoa maelezo ya taasisi hiyo Mkurugenzi wa kanda ya Afrika Mashariki wa MashUbora ambaye pia ni Mkuu wa Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba Dkt. Salma Abdi Mahmoud alieleza kuwa taasisi hiyo ina dhamira ya kuweka Visiwa vya Zanzibar kama eneo kuu la Afrika Mashariki kwa ubora wa utafiti wa kimatibabu.

Kwa upande wake Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa MashUbora alieleza kuwa taasisi hiyo imejitolea kufanya kazi pamoja na serikali chini ya wizara ya Afya Zanzibar ili kusaidia tafiti za kimatibabu, kujengea uwezo wafanyakazi wa kada ya afya katika eneo la kufanya tafiti mbalimbali.
Hata hivyo ameeleza kuwa taasisi hiyo itashirikiana na taasisi za kitaaluma ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar- SUZA, vituo vya huduma za afya, na wadau na jamii ili kuibadilisha Zanzibar kutoka tovuti ya utafiti hadi kituo cha kweli cha utafiti.

Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar ameipokea taasisi hiyo nakuahidi kutoa kila aina ya ushirikiano ili kusaidia kufikia malengo yake hususan kusaidia sekta ya Afya kiutafiti na kuwajengea uwezo watendaji.