The State University Of Zanzibar

SUZA YANGARISHA BONAZA LA HALOTEL 5G

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kushirikiana na kampuni ya Halotel wameendesha Bonaza la Michezo lililowashirikisha Wanafunzi wa kampasi za SUZA, Serikali ya wanafunzi SUZASO na wadau wa michezo Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Skuli ya Afya SUZA, Dkt. Salma Abdi Mahmoud, Afisa Michezo kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Tahir Mkubwa aliwahimiza Vijana kuendelea kufanya mazoezi, ili kuimarisha AFYA zao hali itakayo wasaidia kusoma kwa bidii zaidi.

Bw. Tahir aliwatanabahisha Wanafunzi kuwa, Michezo hutengeneza afya akili, kuimarisha kinga ya mwili, kujenga mashirikiano, kuchangamsha mwili na kujenga uwezo wa fikra katika masomo yao.

“Unapofanya mazoezi ndio unavoweka afya yako vizuri na afya ndio inayo kufanya ukasoma vizuri” alieleza Tahir.

Kwa upande wake Waziri wa michezo SUZASO, Shibli Amour Moh’d, amesema uwepo wa Bonaza hilo ni ishara thabiti ya SUZA inavyowathamini wanamichezo na wanafunzi wake, huku akiahidi kuwa SUZA itaendelea kuratibu Mabonza mengine zaidi yatakayo saidia kuibua vipaji vya wanafunzi.

Aidha aliwashukuru wadhamini wa Bonaza hilo HALOTEL, kwa kuendelea kuunga mkono harakati za michezo za Chuo hicho, nakuwataka wanafunzi kuendela kuiunga mkono Taasisi hiyo.

Tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Skuli ya Afya Mbweni, Mkoa wa mjini Unguja, ambapo michezo mbali mbali ilishuhudiwa ikiwemo mchezo wa Kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mashindano ya kula, Kukimba na ndimu pamoja na mchezo wa mpira wa miguu.

Skuli ya Afya Mbweni ilibuka kidedea katika mchezo wa Mpira wa Miguu, kwa kuifunga bao Moja kwa Sifuri (1:0) Timu ya Kampasi Tunguu, mchezo wa kuvuta kamba Skuli ya Afya mbweni, Wanaume waliibuka kidedea kwa kuwavuta Timu ya Skuli ya Kilimo kizimbani, kwa upande wa wanawake mchezo huo huo, Skuli ya afya mbweni iliibuka tena kidedea kwa kuivuta Skuli ya Kilimo kizimbani.

Washindi wa michezo midogo midogo, Abdul Fatah, kutoka Skuli ya afya mbweni alifanikiwa kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya Kukimbia na ndimu , Khatibu Choum kutoka Kampasi ya Tunguu alifanikiwa kushinda katika mchezo wa kufukuza Kuku, Sleman Juma kutoka Tunguu aliibuka mshindi katika mashindano ya kula na kwa upande wa wanawake katika mashindano hayo Hawa Mohammed kutoka Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba aliibuka kidedea.

Bonaza hilo liliandaliwa na kampuni ya Halotel kwa kushirikiana na SUZA, ili kuibua vipaji pamoja na kutangaza kasi mpya ya matandao huo HALOTEL 5G.