





Zaidi ya Shilingi Bilioni Tisa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Bahari (Chuo cha Ubaharia) cha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), hatua inayolenga kuimarisha sekta ya elimu ya bahari na kuongeza idadi ya wataalamu wazalendo katika nyanja za ubaharia, usafiri wa majini, na uchumi wa buluu.
Ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kutoa fursa kwa vijana wengi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupata elimu na mafunzo ya kitaalamu yatakayokidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi. Kupitia chuo hicho, wanafunzi watapatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo katika maeneo ya uongizaji wa vyombo vya majini, usalama baharini, uendeshaji wa vyombo vya majini, pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za bahari.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ndg. Khamis Said Abdulla, amesema kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane unaolenga kuendeleza uchumi wa buluu na kuitumia kikamilifu fursa ya kijiografia ya Zanzibar kama kitovu cha bahari na biashara ya kimataifa.
Aidha, ujenzi wa Chuo cha Ubaharia cha SUZA unatarajiwa kuongeza uwezo wa taasisi hiyo katika kufanya tafiti za masuala ya bahari, na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za uvuvi, usafiri wa baharini, na utalii wa baharini.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuinua elimu ya juu nchini, kukuza rasilimali watu, na kuwaandaa vijana ili waweze kushindana kikamilifu katika soko la ajira la ndani na la kimataifa.