The State University Of Zanzibar

WEMA yasaini mkataba Ujenzi Taasisi Mafunzo ya Bahari

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetiliana saini na kampuni ya Ms TIL Construction Limited mkataba wa ujenzi jengo la Taasisi ya Mafunzo ya Bahari ulioko chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) chini ya Mradi wa Kuwajengea Uwezo Vijana  Kujiajiri na Kuajirika  Kupitia Uchumi wa Buluu (SEBEP).

Ujenzi huo utajumuisha jengo ya utawala, zikiwemo ofisi za walimu, madarasa ya kufundishia kwa vitendo, karakana ya mafunzo ya kuzima moto na bwawa la kuogelea umepangwa kukamilika ndani ya miezi 18.

Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini, katika ofisi za makao makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mazizini mjini Magharibi Unguja tarehe 2/01/2026, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw.  Khamis Abdulla Said alisema mradi huo  unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika   unalenga  kutatua changamoto kwenye sekta ya bahari.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo  itakuwa na miundombinu ya kisasa itakayofundisha masuala yote yanahusu bahari na kusajili wanafunzi wa ndani na  nje ya nchi wanaosomea fani mbali mbali zinazohusu bahari.

Katibu Mkuu alifahamisha kuwa Wizara anayoiongoza ina matumaini makubwa ya kuwa watakamilisha kazi hiyo ndani ya miezi 16 na endapo watafanikiwa hivyo na kukabidhi kazi yenye viwango, Kampuni. hiyo itakuwa ni mkandarasi wao wa kudumu.
‘’Baada ya mradi huu kutakuwa na mradi wa ujenzi wa Vyuo vya Amali vitano’’, alisisitiza Katibu
Mkuu.
Aidha, alimkumbusha mkandarasi huyo  kuwaajiri vijana wazawa katika fani zote wanazozihitaji na kuwaruhusu  kuchukua vijana kutoka nje kwa zile fani ambazo wazawa hawatakuwa nazo. ‘’ Tukijenga haraka kuna kozi tano ambazo lazima zisomeshwe kama vile huduma ya kwanza, uokozi na kuzima moto ambapo  wanafunzi wanazipata katika vyuo vyengine vya nje’’, alisema.

Meneja Msimamizi wa Kampuni hiyo ya Till Construction,  Bw. Faraji Selemani aliahidi kuwa Kampuni   yake  itakamilisha kazi hiyo na kuikabidhi kabla ya muda wa miezi 18 iliyowekwa. Mapema, Meneja wa Mradi wa SEBEP, Bw. Salum Mkubwa Abdallah alifahamisha kuwa kampuni 21 zilinunua nyaraka za zabuni hiyo na kampuni ya Ms TIL Construction Limited ilishinda zabubuni hiyo yenye gharama ya shilini bilioni 9,167,458,454.1/.