





WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, amewasihi wahitimu na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuitumia fursa waliyonayo kubuni miradi itakayowawezesha kujiajiri badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.
Nasaha hizo alizitoa wakati akizungumza kwenye Mkusanyiko wa Tatu wa Kitaaluma uliofanyika tarehe 13/12/2025 Taasisi ya Utalii katika Kampasi ya SUZA Maruhubi.
Aliwaambia wanapomaliza kusoma wanakuwa wamemaliza muhula tu wa kukaa darasani lakini maisha mapya yanayohitaji elimu na taaluma waliyoipata inaanza baada ya masomo.
‘’ Mnapomaliza msiwe sehemu ya kutafuta ajira, fikirieni mambo yatakayowawezesha kutatua changamoto zinazoikabili jamii’’, alifahamisha.
Vile vile aliwakumbusha umuhimu wa kuitambua kuwa hata wanapomaliza masomo wajue wao ni zao la SUZA na hivyo wanapaswa kushiriki vyema katika shughuli zote za kijamii.
Nae Kaimu Makamu Mkuu wa SUZA Prof. Abdi Talib alisema dira ya Chuo hiki ni kuifanya kuwa taasisi bora ya elimu ya juu na utafiti ikienda sambamba na kauli mbiu kuwa SUZA ni kichocheo cha mabadiliko ya jamii.
Aidha, lengo la kuanzishwa mkusanyiko huu ni kuonesha ushirikiano wa wahitimu, walimu na wadau wote kuwa wana mchango mkubwa,
kuchochea mabadiliko chanya katika jamii na kutumia mfumo wa kidigitali na kubadilishana uzoefu wa vyuo.
Nae mwenyekiti wa mkusanyioko huu Convocation Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma wanafunzi hao na kuwapongeza kwa namna walivyofanya vizuri kwenye masomo yao ambapo baadaye walipewa vyeti na zawadi.
Katika mkusanyiko huo , washiriki walipata fursa ya kusikiliza na kuchangia mada inayohusiana na masuala ya ujasiriamali wa jamii na ubunifu kwa ajili ya kuunda ajira endelevu.