







Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Salum Seif Salum amewahimiza waratibu wasimamizi wa vikao wa SUZA, kuleta mabadiliko yatakayo saidia kukuimarisho Chuo hicho.
Amezungumza hayo wakati wa ufungaji wa Mafunzo hayo kwa niaba ya Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Abdi Talib Abdalla katika ofisi za Makao Makuu SUZA , Tunguu wakati alipofunga Mafunzo ya siku Nne (4) waratibu hao, ya kuzingatia itifaki, uendeshaji wa vikao, uchukuaji wa kumbukumbu za mikutano, kukaribisha wageni na kuwahudumia na kanuni za kuendesha vikao.
Prof. Salum aliwataka waratibu hao kuzingatia mafunzo waliopewa, kutekeleza majukumu yao kwa misingi ya kisheria kama walivyoelekezwa katika mafunzo hayo pamoja na kuwa mabalozi wazuri kwa wafanyakazi wenzao.
Aidha alitumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa mwendesha mafunzo, Bw. Josephat Buhenyenge, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumuahidi kuwa SUZA itayafanyia kazi mafunzo yote aliyoyatoa.
Kwa upande wake mwendesha mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Mwandamizi Utawala kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Bw. Josephat Buhenyenge, alitoa shukrani zake kwa SUZA, na kuahidi kwamba wakati wote atakua bega kwa bega na kuunga mkono harakati zote maendelo zitakazofanyika ndani ya Chuo hicho.
Nao baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yamesaidia kuonesha pengo lililopo na yatasaidia kuziba pengo hilo.
Mafunzo hayo ya siku Nne yalianza tangu Januari 21, 2026 na kutamatika Januari 24, 2026.