






Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeendelea kuimarisha uhusiano wa kimataifa kupitia mikataba na mashirikiano na taasisi mbalimbali za elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na kukuza ubora wa elimu inayotolewa.
Akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Virginia Commonwealth University – School of the Arts, Qatar, iliyofanyika katika kampasi ya Tunguu, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati Unguja, Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji, alieleza kuwa SUZA ina historia ya ushirikiano kubwa unaolenga kukuza maarifa na utafiti katika sekta mbalimbali za elimu. Aliifafanua zaidi kuwa ushirikiano wa kimataifa ni sehemu muhimu ya dira ya Chuo katika kufanikisha maendeleo ya elimu ya juu nchini.
Prof. Moh’d Makame Haji alieleza kuwa kwa sasa SUZA ina skuli tisa, zikiwemo Skuli ya Biashara, Skuli ya Kilimo, Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Skuli ya Meno, Skuli ya Kompyuta na Mawasiliano ya Habari, Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, Skuli ua Elimu, Skuli ya Sayasi Jamii na Sayansi Asili, Skuli ya Elimu Endelevu na Utaalamu pamoja na taasisi mbili za kitaaluma ambazo ni Taasisi ya Utalii na Taasisi ya Mafunzo ya Bahari.
Katika mazungumzo hayo, Prof. Moh’d Makame Haji alisisitiza umuhimu wa kuandaa hati rasmi ya makubaliano (MoU) kati ya SUZA na Virginia Commonwealth University Qatar, ili kuendeleza ushirikiano kwa faida zaidi, hasa katika maeneo ya ubunifu na elimu ya utalii.
Dkt. Neelima Jeychandran kutoka Virginia Commonwealth University School of the Arts in Qatar (VCU Qatar) ameipongeza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa mapokezi ya kipekee na maelezo ya kina kuhusu maendeleo ya taasisi hiyo. Akizungumza katika kikao rasmi, Dkt. Jeychandran alieleza kuwa VCU Qatar iko tayari kuendeleza ushirikiano na SUZA, hususan katika nyanja za historia, makumbusho na utamaduni, maeneo ambayo alisisitiza kuwa yana fursa nyingi za kitaaluma na kijamii.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilijadili uwezekano wa kuandaa tafiti za pamoja, kubadilishana wataalamu, na kushiriki katika makongamano ya kitaifa na kimataifa. Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kitaaluma kati ya taasisi hizo mbili na kuchangia katika kukuza maarifa na utamaduni wa Zanzibar na kanda ya Ghuba.