





Naibu Katibu Mkuu – Sayansi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel E. Mushi, amewataka wakandarasi wanaoshughulikia ujenzi wa majengo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuongeza kasi ya ujenzi kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi na muda wa kazi, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya maabara na jengo la Skuli ya Kilimo katika kampasi ya Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, Prof. Daniel E. Mushi alisisitiza kuwa mradi huo ni wa kimkakati na unatekelezwa kwa ufadhili wa Benk ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.
“Huu ni mradi wa wananchi. Fedha zinazotumika hapa ni za walipakodi, hivyo ni lazima tuhakikishe unakamilika kwa wakati ili kuepuka gharama zisizo za lazima,” alisisitiza Prof. Daniel E. Mushi.
Alieleza kuwa mradi wa HEET ulianzishwa kutokana na ongezeko la wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, jambo lililohitaji maboresho ya miundombinu katika taasisi za elimu ya juu. Mradi huu pia unalenga kuboresha mitaala, huduma za TEHAMA, na kuwajengea uwezo wakufunzi ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kisasa.
Prof. Mushi alipongeza SUZA kwa hatua kubwa iliyofikia katika utekelezaji wa mradi huo na akaonesha matumaini kuwa usimamizi wa karibu utaendelea kuhakikisha ujenzi unamalizika mwezi Juni, 2026 kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Dkt. Haji Ali Haji, msaidizi mratibu wa Mradi wa HEET – SUZA kwa niaba ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha, Mipango na Utawala, Dkt. Hashim Hamza Chande, alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta ongezeko la nafasi kwa wanafunzi wapya katika Chuo hicho
“Mradi huu utakapo kamilika utaongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi wengi zaidi na kutoa mafunzo ya kisasa yanayokidhi mahitaji ya taifa,” alisema Dkt. Haji Ali Haji.
Naye Mratibu wa kampuni inayosimamia ujenzi wa majengo hayo, Joakim Modest, alieleza kuwa wamejipanga kuongeza idadi ya wafanyakazi pamoja na muda wa kazi ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
“Tumejipanga kuongeza nguvu kazi na muda wa kazi, ili kufikia malengo ya kukamilisha ujenzi ndani ya muda uliowekwa,” alisema Joakim Modest.
Majengo haya mapya yanayojengwa katika kampasi ya Tunguu yanatarajiwa kubadilisha sura ya utoaji elimu ya juu Zanzibar na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kitaaluma na kiuchumi ya taifa kwa ujumla. Ziara hii imefanyika Leo tarehe 26/09/2025 Kampasi ya Tunguu