Skip to main content

The State University Of Zanzibar

WAHITIMU WA MAFUNZO YA KIDIJITALI KUPITIA MRADI WA HEET WATAKIWA KUTUMIA UJUZI KATIKA SOKO LA AJIRA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Prof. Said Ali Hamad Vuai, amewataka wahitimu wa mafunzo ya kidijitali kupitia Mradi wa HEET kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kama fursa ya kujiandaa na kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.

Prof. Vuai ameyasema hayo Jumanne, tarehe 6 Oktoba 2026, wakati wa hafla ya ugawaji wa vyeti kwa wahitimu wa mafunzo hayo yaliyodumu kwa siku nne, iliyofanyika katika Ukumbi wa SMH SUZA.

Amesema dunia ya sasa haiangalii vyeti pekee, bali inahitaji watu wenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kutumia kile walichojifunza katika mazingira halisi ya kazi.

“Dunia ya leo ina mambo mengi na inahitaji vijana wenye ujuzi unaoweza kutumika katika mazingira halisi ya kazi,” amesema Prof. Vuai, huku akiwataka wahitimu kutumia taaluma na maarifa waliyoyapata kuongeza uwezo wao na kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya soko la ajira.

Aidha, Prof. Vuai amewataka wahitimu kuendelea kujifunza na kujiendeleza zaidi katika eneo la teknolojia na ujuzi wa kidijitali, akisisitiza kuwa mafunzo hayo yanapaswa kuwa mwanzo wa safari ya kujenga uwezo zaidi wa kitaaluma na kiutendaji.

Amewapongeza wahitimu kwa kushiriki katika mafunzo hayo na kuwataka kutumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa yao binafsi, taasisi wanazofanyia kazi pamoja na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Abdi Talib Abdalla, amewataka wahitimu kutumia ipasavyo nyenzo na ujuzi wa kidijitali walioupata ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao na kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

Prof. Abdi amesema ujuzi wa kidijitali una nafasi muhimu katika kuboresha utendaji kazi, hivyo wahitimu wanapaswa kuhakikisha wanatumia maarifa hayo katika kutatua changamoto na kuleta matokeo chanya katika jamii.

Vilevile, amewataka wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa taaluma walizojifunza pamoja na kuwa mabalozi wazuri wa SUZA kwa kutumia ujuzi huo kwa manufaa ya jamii na kuchangia katika maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Naye Mkuu wa Mradi wa HEET amesema mafunzo hayo ya kidijitali ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa HEET unaohusisha vyuo sita, ukiwa na lengo la kuwawezesha washiriki kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya teknolojia na mabadiliko ya dunia ya sasa.

Amesema mafunzo hayo yamewalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kutumia teknolojia na zana mbalimbali za kidijitali katika kuboresha utendaji wao na kuongeza ushindani katika soko la ajira.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za SUZA kupitia Mradi wa HEET katika kuwawezesha washiriki kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya soko la ajira. Ujuzi uliopatikana unatarajiwa kuwasaidia wahitimu kuongeza ufanisi katika kazi zao, kuibua fursa mpya za kiuchumi na kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kitaaluma.