

























Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu Zanzibar (BASSF), kinatarajia kuanzisha Skuli ya Sanaa itakayotoa elimu na mafunzo ya kitaaluma kwa wasanii, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya sanaa, kuinua hadhi ya wasanii na kukuza mchango wa sanaa katika uchumi na maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu nafasi ya sanaa katika uchumi na maendeleo ya Zanzibar, uliofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Kampasi ya Tunguu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ndg. Matar Zahor Masoud, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya sanaa kwa kuwapatia wasanii elimu na ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi zao kwa weledi na viwango vya kitaaluma.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia wasanii kubobea katika fani zao, kuongeza ubora wa kazi zao na kutumia vipaji walivyonavyo kama nyenzo ya kujipatia kipato na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.
Aidha, amewataka washiriki wa mdahalo huo kutumia fursa hiyo kueleza changamoto zinazowakabili, kubadilishana uzoefu na kutoa maoni pamoja na mapendekezo yatakayosaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza sekta ya sanaa.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdalla, amesema chuo hicho kitashirikiana na BASSF katika kufanya tafiti, kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wasanii pamoja na kuanzisha vituo vya kukuza vipaji na ubunifu.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kubadilisha mawazo na vipaji vya wasanii kuwa bidhaa na huduma zenye thamani ya kiuchumi, hivyo kufungua fursa zaidi za ajira na kujiajiri kwa vijana na makundi mengine yanayojihusisha na sanaa.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Kati, Mhe. Rajab Ali Rajab, amewataka wasanii kuzingatia nidhamu, juhudi, ubunifu na maarifa katika shughuli zao za kisanaa, huku akiwahimiza kuwa tayari kujifunza na kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.
Amesema Zanzibar ina vipaji na vikundi vingi vya sanaa katika maeneo mbalimbali, hivyo ni muhimu wasanii kupata elimu na mafunzo yatakayowawezesha kuendeleza vipaji vyao, kuongeza weledi na kufikia viwango vya juu zaidi katika kazi zao.
Mdahalo huo wa Kitaifa umefanyika ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), yanayolenga kutathmini mafanikio ya chuo hicho na kuimarisha mchango wake katika elimu, utafiti, ubunifu na maendeleo ya Zanzibar pamoja na Taifa kwa ujumla.
