Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimezindua rasmi maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo, yanayolenga kusherehekea safari ya mafanikio, kutathmini hatua za maendeleo zilizofikiwa na kuweka msingi wa maendeleo zaidi katika miaka ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano, Makao Makuu ya SUZA, Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Said Ali Hamad Vuai, amesema maadhimisho hayo yatahusisha matukio mbalimbali ya kitaaluma, kijamii, michezo na maendeleo yatakayowashirikisha wanajumuiya wa SUZA pamoja na jamii kwa ujumla.
Prof. Vuai amesema maadhimisho hayo yameandaliwa kwa lengo la kuadhimisha safari ya miaka 25 ya Chuo, kutambua mchango wa wanajumuiya mbalimbali katika maendeleo ya SUZA, pamoja na kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika nyanja za elimu, utafiti, ubunifu, huduma kwa jamii na maendeleo ya Chuo.
Ametaja baadhi ya shughuli zitakazofanyika katika kipindi cha maadhimisho hayo kuwa ni pamoja na dua maalumu ya kuwaenzi wanajumuiya wa SUZA waliotangulia mbele ya haki, matembezi ya hisani, bonanza la michezo, makongamano, Wiki ya Kiswahili, shughuli za kijamii pamoja na maonesho ya utafiti na ubunifu.
Matukio mengine ni Wiki ya Convocation, Mahafali ya 22 ya Chuo, uzinduzi wa vitendea kazi pamoja na uzinduzi wa Mfuko Maalumu wa Maendeleo ya Chuo, ambao unalenga kusaidia ujenzi wa jengo la Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba.
Sambamba na hayo, Prof. Vuai amesema maadhimisho hayo yatahusisha pia shughuli za upandaji miti, usafi wa mazingira, huduma za afya ya kinywa na meno pamoja na kampeni mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kijamii.
Aidha, Prof. Vuai ametoa wito kwa jamii, wafanyabiashara, watu mashuhuri, Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), wanasiasa na wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana na SUZA kwa kuchangia fedha katika ujenzi wa jengo la Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba.
Amesema ujenzi wa jengo hilo ni muhimu katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuongeza uwezo wa Chuo kutoa programu za afya na sayansi za tiba, pamoja na kuwawezesha wanafunzi kupata elimu hiyo Zanzibar. Hatua hiyo, amesema, itasaidia kupunguza gharama zinazoweza kuepukika kwa wanafunzi wanaolazimika kwenda nje ya Zanzibar kutafuta elimu katika fani hizo.
Kwa upande mwingine, maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa SUZA kuendelea kuimarisha uhusiano na jamii, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wadau mbalimbali katika kuendeleza elimu ya juu na kuchochea maendeleo ya Zanzibar.
Maadhimisho ya Miaka 25 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yamezinduliwa rasmi leo, tarehe 6 Oktoba 2026, na yatahusisha shughuli mbalimbali zinazolenga kutafakari safari ya Chuo, kuonesha mafanikio yaliyopatikana, kutambua mchango wa wadau wake na kuweka msingi wa hatua mpya za maendeleo kwa miaka ijayo.
