Skip to main content

The State University Of Zanzibar

SUZA, WEMA KUIMARISHA ELIMU JUMUISHO ZANZIBAR.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata haki na fursa sawa za kupata elimu nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Elimu Jumuishi Zanzibar (ZIIES 2026), lililofanyika katika Hoteli ya Madinatul Bahar, Mbweni, Mjini Zanzibar, Mheshimiwa Othman amesema Serikali itaendelea kuimarisha elimu jumuishi kwa kuhakikisha wanafunzi wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata elimu bora katika mazingira rafiki na yanayozingatia mahitaji yao.

Ameeleza kuwa kufanikisha azma hiyo kunahitaji kuboresha sera za elimu, kuwaandaa walimu wenye ujuzi wa elimu jumuishi, kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na kutumia mbinu sahihi za ufundishaji zinazozingatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.

Aidha, amesema Serikali tayari imeanza kuchukua hatua kwa vitendo ikiwemo kuajiri walimu waliopata mafunzo ya elimu jumuishi pamoja na kuboresha vifaa vya kufundishia ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Mboja Ramadhan Mshenga, amesema Wizara yake iko tayari kupokea maoni na michango ya wadau mbalimbali kupitia kongamano hilo kwa lengo la kuboresha Sera ya Elimu Zanzibar ili iendane na mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Naye Mkuu wa Skuli ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Said Khamis Juma, amesema SUZA inapoadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwa taasisi inayochochea mabadiliko ya kijamii kupitia elimu na tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Amesema SUZA inajivunia kuwa miongoni mwa taasisi zilizoandaa kongamano hilo, akieleza kuwa majadiliano yatakayofanyika yatatoa mchango muhimu katika kuboresha Sera ya Elimu Jumuishi Zanzibar na kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa wote.

Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Norway Association of Disabled (NAD), Shirikisho la Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHUJUWAZA), Madrasa Early Childhood Programme Zanzibar pamoja na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

10 Novemba 2026