












Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendesha mafunzo maalum ya uelewa kuhusu matumizi ya ndege zisizo na rubani, yaliyolenga kuwaongezea uelewa wadau kuhusu sheria, taratibu na matumizi salama ya teknolojia hiyo.
Mafunzo hayo yamewakutanisha viongozi wa Shehia ya Jumbi, akiwemo Sheha na wajumbe wake, watumiaji na wadau wa ndege zisizo na rubani kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), pamoja na maafisa kutoka Jeshi la Polisi.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na salama ya ndege zisizo na rubani, hususan katika kipindi ambacho matumizi ya teknolojia hiyo yanaendelea kukua.
Dkt. Bakari amesema ukuaji wa matumizi ya ndege zisizo na rubani unahitaji watumiaji na wadau kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na taratibu zinazowaongoza, ili kuhakikisha matumizi yake hayahatarishi usalama wa usafiri wa anga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Skuli ya Kompyuta, Mawasiliano na Masomo ya Habari , SUZA, Prof. Abubakar Diwani Bakari, amesema SUZA imekuwa na historia ya kushiriki katika matumizi na maendeleo ya teknolojia ya ndege zisizo na rubani.
Prof. Bakari amesema kuwa SUZA ilishiriki katika mradi wa “Zanzibar Mapping Initiatives” uliofanyika mwaka 2016–2017, ambapo SUZA pia ilikuwa na maabara maalum ya ndege zisizo na rubani, iliyosaidia kukuza matumizi ya teknolojia hiyo katika tafiti na shughuli mbalimbali za kitaaluma.
Amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wadau mbalimbali kwa kuwa yanawawezesha kuelewa namna sahihi ya kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani kwa kuzingatia sheria, taratibu na usalama.
Mafunzo hayo yamejikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo sheria na kanuni zinazosimamia matumizi ya ndege zisizo na rubani, taratibu za kuingiza ndege hizo nchini, usajili, upatikanaji wa vibali pamoja na wajibu wa watumiaji kuhakikisha matumizi yake hayakiuki usalama wa usafiri wa anga.