The State University Of Zanzibar

Prof. Hikmany aongoza ziara ya kikazi SUZA

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Profesa Hamed R.H. Hikmany, amefanya ziara ya kikazi na kukutana na wafanyakazi wa Kurugenzi, Idara na Vitengo mbalimbali vya Chuo.

Lengo kuu la ziara hii ni kujua majukumu na utekelezaji wa shughuli za kila siku za Chuo, pamoja na mafanikio na changamoto zinazoikabili SUZA. Akiwa ameongozana na viongozi na wajumbe wa Baraza la SUZA akiwemo Bi. Salma H. Saadat, Prof. Abdi Talib Abdalla Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Salum Seif Salum  Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Dkt. Mtaib Abdulla Othman Katibu wa Baraza la Chuo.

Katika mazungumzo yake, Prof. Hikmany alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto zilizopo ili kuharakisha utoaji wa huduma bora za kitaaluma, utafiti, ushauri elekezi na uendeshaji kwa jamii. Aidha aliwataka watumishi wa Chuo kuachana na tabia za kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuzingatia ubunifu na uwajibikaji.

Mwenyekiti alisisitiza dhamira ya Baraza kuhakikisha SUZA inabaki kuwa kinara wa elimu ya juu Zanzibar. Ziara ya leo tarehe 6 Mei, 2026 ilihusisha mikutano na watendaji wa Kurugenzi ya Rasilimali Watu, Kurugenzi ya Mali za Chuo na Huduma, Idara ya Mipango, Sera na Takwimu, pamoja na Idara ya Huduma za Sheria.

Prof. Hikmany aliteuliwa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la SUZA mnamo tarehe 19 Januari, 2026.