The State University Of Zanzibar

SUZA na UGHE kushirikiana kuzalisha wataalamu wabobezi wa afya

Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kitaaluma na Chuo Kikuu cha Global Health Equity (UGHE) cha Rwanda, kwa lengo la kuboresha huduma za afya na kuinua ubora wa elimu katika sekta hiyo kwa pande zote mbili.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Abdi Talib Abdalla, amesema SUZA iko tayari kushirikiana na UGHE katika kubadilishana uzoefu na utaalamu, ili kuzalisha wataalamu vijana waliobobea katika fani mbalimbali za afya.

Prof. Abdalla aliyasema hayo alipokutana na ujumbe wa watu wanne kutoka UGHE, ukiongozwa na Bi. Masimbi Ornella, Mkuu wa Kitivo cha Teknolojia za Uigaji, katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya SUZA, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, tarehe 4 Novemba 2025.
Amesema ushirikiano huo utakuwa endelevu na utaangazia kubadilishana utaalamu kati ya walimu na wanafunzi wa pande hizo mbili, jambo litakalosaidia kuinua viwango vya elimu na utafiti katika nyanja ya afya.

Kwa upande wake, Bi. Ornella amemhakikishia Prof. Abdi Talib Abdalla kuwa UGHE imejipanga kutoa ushirikiano wa karibu na SUZA, hususan katika kuimarisha taaluma ya utabibu, huduma za kimaabara, pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto.

Ameeleza kuwa chuo chake kimekuwa kikishirikiana na taasisi mbalimbali barani Afrika ikwemo Congo, Uganda, Liberia, Nigeria, Zanzibar na nk pamoja na kutoa udhamini wa masomo ya udaktari, huku kikiweka mkazo maalum kwa wanafunzi wa kike ili kuwapa nafasi zaidi katika sekta ya afya.
Aidha, amewahimiza wanafunzi kutoka Zanzibar kutumia fursa zinazotolewa na UGHE kwa kuomba udhamini wa masomo, ili kuchangia katika kufikia malengo ya kutoa huduma bora na zenye ubunifu katika sekta ya afya.