The State University Of Zanzibar

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Prof. Moh’d Makame Haji amewataka vijana wasomi nchini kuhakikisha wanaendeleza falsafa zilizoachwa na waasisi wa taifa letu kwa lengo la kuleta maendeleo

Akizungumza katika mkutano na viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu katika ukumbi wa mikutano Tunguu amesema kuwa, vijana Wana Kila sababu ya kuendeleza falsafa zilizoachwa na waasisi ikiwemo ukombozi wa watu na jitihada za kuleta maendeleo.

Amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kutoa taarifa kuhusu kongamano la Kigoda cha Taaluma cha Hayati Abeid Amani Karume lenye lengo la kuenzi falsafa zake na kuwakutanisha pamoja wasomi kwa kutathmini mambo ya msingi yanayoihusu ustawi wa taifa yatakayoweza kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyengine Prof. Makame amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza miaka mitano katika uongozi wake ambao umeleta mabadiliko makubwa nchini ikiwemo wanafunzi kunufaika na mikopo ya elimu ya juu katika sekta ya elimu.

Nae Mkuu wa Skuli ya Sayansi Asilia na Sayansi Jamii Dkt. Abdala Mkumbuka amesema kuwa kongamano hilo litakuwa ni la muendelezo ambalo limewalenga wasomi vijana ili kutambua falsafa za viongozi waliopita kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, siasa na uchumi kutokana na vijana kuwa chachu ya kuleta maendeleo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Serikali za Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Zanzibar wamewataka vijana wasomi kutumiya taaluma zao kwa kutatua changamoto na kuleta maendeleo nchini bila ya kukubali kufata mkumbo wa kusababisha vurugu kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu pamoja na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wanafunzi wenzao ili kunufaika na Kigoda hicho.

Kongamano la Kitaaluma la Kigoda cha hayati Abeid Amani Karume linatarajiwa kufungukiwa na Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi na kauli mbiu ni “Maisha ya Sheikh Abeid Amani Karume na Urithi kwa Vijana, Amani, Mshikamano na Demokrasia kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025”.