The State University Of Zanzibar

SUZA, UNICAM kuendeleza ushirikiano kitaaluma

VIONGOZI wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Camerino (UNICAM) cha Italia wamejadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano wa kitaaluma ili kuongeza kasi maendeleo kwenye nyanja ya elimu na kutoa wahitimu waliobobea kwenye program wanazotoa.

Vyuo hivyo viwili vilitiliana saini mkataba wa ushirikiano mwaka 2019 katika taaluma kwa kubadilishana wanafunzi, kufanya tafiti za pamoja na mambo emgnine ya kielimu.

Wakizungumza katika ofisi ya makao makuu ya SUZA yaliyopo Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 24/06/2025 viongozi hao, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, prof. Moh’d Makame Haji na Prof. Cristina Micel wa Skuli ya Sayansi na Wanyama katika Chuo cha Camerino walikubaliana kuendeleza ushirikiano wao kwa miaka mingine mitano ijayo.

Katika mkataba uliopita SUZA imefanikiwa kuteua wanafunzi bora wawili wamebahatika kuendelea na masomo yao ya Shahada ya pili nchini Italia na wanatarajiwa kuhitimu mwezi Oktoba mwaka huu wakati wafanyakazi wengine wawili wa Skuli ya Afya wamefanikiwa kuendelea na masomo nchini humo.

Katika utekelezaji wa mkataba mpya, washirika hawa wataendesha semina ya pamoja ambayo itawajumuisha walimu kutoka Italia na Zanzibar itakayojumuisha pia wadau wengine wanaoshughulikia masuala ya afya.

Hali kadhalika ushirikiano huu hautaishia kwenye Nyanja ya afya pekee bali utazingatia pia masuala ya kilimo na sayanasi asilia. Aidha, wamekubaliana kuwepo na ubadilishanaji wa wanafunzi kwa miezi miwili ambapo Skuli ya Afya tayari imewasilisha majina ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza porgramu hiyo kuanzia mwezi wa Septemba.