The State University Of Zanzibar

Wadau wapitia rasimu mafunzo usalama wa bahari

WADAU kutoka taasisi zinazoshughulikia masuala ya bahari Tanzania wamepitia rasimu ya mtaala wa mafunzo ya usalama wa bahari ili kuwawezesha kuitumia rasilimali hiyo kwa maendeleo endelevu.

Akifungua kikao kilichofanyika makao makuu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) tarehe 24/06/2025, Makamu Mkuu wa chuo hiki alisema hatua hii ni muhimu kufanyiwa kazi ipasavyo kwani Chuo kinatekeleza mipango mikuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kila mmoja anapaswa kutoa mchango wake kufikia malengo iliyojiwekea.

Alifahamisha kuwa katika kufikia malengo hayo, nchi imepitisha Sera ya Uchumi wa Buluu mwaka 2020 na kuipitia mwaka 2022 ambayo imeongeza kasi ya kupanua wigo wa matumizi ya rasilimali za bahari na kutoa elimu.

“Tunafahamu umuhimu katika masuala ya mawasiliano kutembeleana, biashara, usafirishaji, kutuma na kuagiza na yanayohusiana na uelewa maeneo ya huduma kama vile malazi matembezi afya na maengine kadhaa yote haya yanaunganishwa kwa maingiliano

Hata hivyo, aliongeza kuwa utekelezaji ulianza mapema ingawaje pole pole na kuongezeka baada ya kupata mradi wa SEBEP ambao ulizingatia uhitaji wa vijana katika kutumia fursa zinazopatikana kwenye raslimali ya bahari kupatiwa uwezo na nyenzo watakazozitumia kwa kujipatia kipato na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha alieleza matumizi mengi na muda mrefu ya rasilimali ya bahari bila ya kuwa na weledi na utambuzi huku jamii ikitambua kuwepo vijana wengi mabaharia waliobobea lakini hawatambulikani kimataifa zaidi ya jamii inayowazunguka.

Aliongeza kuwa lengo jengine lilisukuma kuwa na program kama hizi ni kuwaongezea uwezo vijana waliopo na wanaokuja baadaye kwa kupewa program zinazotambulikana kimataifa na kuwapa nguvu ya kufanya kazi zao.

Akizungumzia kuhusu washiriki waliopitia rasimu hiyo, Prof. aliwaambi kuwa wamalikwa ili kuchangia mawazo kwenye maudhui yaliyomo kweny rasimu hiyo iendane na uhalisia wa jambo lilikusudiwa.

Akimkaribisha Prof. Haji. Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Mafunzo ya Bahari ya SUZA, Bw. Yahya Hamad Sheikh alisema mitaala hii imetengenezwa kwa mujibu wa muongozo wa Shirika la Bahari Duniani.

“Pamoja na muongozo wa kimataifa, zaidi ya asilimia 80 ya maudhui ya rasimu hii inatokana mazingira yanayotuzunguka na pia kwa kuzingatia mahitaji ya nchi yetu’’, alisisitiza Dk. Yahya.

Alifahamisha utekelezaji wa mtaala huu unatarajiwa kufanyiwa kazi hivi karibuni kutokana kuwa na maandalizi ya kutosha kutoa taaluma hii.

Kikao hicho kimewakutanisha wataalamu mbali mbali wakiwemo mabaharia, madaktari ambao watafundisha huduma ya kwanza, waendesha meli, wahandisi wa meli, wataalamu wa zimamoto, wanasheria na wataalamu wengine katika sekta ya usafirishaji kinakwenda sambamba na Wiki ya Mabaharia Duniani.