


Kituo cha Center for Digital Learning (CDL) cha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kwa kushirikiana na Taasisi ya Shule Direct ya Tanzania, kimeingia katika ushirikiano wa kimkakati kutekeleza Mradi wa Virtual Learning Environment (VLE) wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ikiwa ni jitihada mahsusi za kuimarisha sekta ya elimu kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Akizungumza wakati wa kikao na uongozi wa SUZA kilichofanyika kampasi ya Tunguu, Meneja wa Shule Direct, Bi Faraja Kota, alieleza kufurahishwa kwake na nafasi ya taasisi yao katika utekelezaji wa mradi huu wa kitaifa. Alisema, “Tuna uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika nyanja ya elimu ya kidijitali—tuna wataalamu, miundombinu rafiki na mazingira mazuri ya kazi. Tunatarajia mradi huu kuleta mabadiliko makubwa katika mazingira ya kujifunza.”
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa SUZA, Profesa Moh’d Makame, alisisitiza kuwa ushiriki wa chuo katika mradi huu ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha huduma za elimu kupitia TEHAMA. Alieleza kuwa SUZA inatilia mkazo matumizi ya akili undena kanzidata kwa manufaa ya jamii, na akasisitiza kuwa, “Elimu ni kichocheo muhimu kwa maendeleo ya taifa. Bila elimu, hatuwezi kupiga hatua ya kweli.
Aliongeza kuwa kupitia utekelezaji wa mradi huu, SUZA inalenga kuwajengea wanafunzi ujuzi wa matumizi ya teknolojia ya kisasa na maarifa ya kisayansi, kwa kuendana na mahitaji halisi ya soko la ajira. Pia alipongeza jitihada za kuwajengea uwezo wataalamu wa wizara, maafisa elimu wa mikoa, na watendaji wengine, ili kuhakikisha mafanikio endelevu ya mradi huu.