


CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeunda ushirikiano wa kitaaluma na Chuo Kikuu cha Misri cha Sadat City (USC) ambapo kinatarajia kufungua tawi la Chuo hicho kitakachokuwa na ofisi zake katika kampasi za SUZA.
Akizungumza katika hafla fupi ya kujadiliana namna ya kutekeleza ushirikiano huo, Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji, alisema amepokea kwa furaha wazo la kuanzishwa kwani tawi hilo kwani litapanua wigo kitaaluma.
‘’Nina furaha kwani hatua hii itaifanya SUZA kupokea wanafunzi kutoka nchi nyingi za kigeni lakini pia kuongeza maeneo ya ushirikiano’’, alisema Prof.
Aidha, aliongeza kuwa ushirikiano huo utakuwa wa aina yake kwabvile kuna mambo mengi ambapo vyuo hivi viwili vinafanana hasa katika utoaji wa taaluma kwenye prpgram mbali mbali.
Alifahamisha kuwa miongoni mwa program zinazotolewa katika vyuo hivyo ni pamoja na masuala ya afya, dawa, utalii, kilimo, biashara, teknolojia ya Akiliunde, sambamba na lugha ambapo SUZA imeongeza wigo wa utoaji wa taaluma za lugha kwa kuongeza program ya Lugha ya Kiarabu kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Naye Rais wa Chuo hicho, Prof. Shaden Muawia alisema kuanzishwa kwa Kampasi ya USC SUZA kutapunguza gharama kwa wanafunzi wa Tanzania kwenda Egypt, Misri na kuvutia wanafunzi wengine kuja Zanzibar.
Alisema asilimia 30 ya wanafunzi wanaojiunga kwa mwaka huwa wanatoka katika nchi za kiafrika ikiwa ni pamoja na Zambia na Zimbabwe huku Tanzania ikiongoza kuwa na wanafunzi wengi.
‘’Tunaamini kuwa wanafunzi wengi watavutiwa kuja hapa, sisi tunapenda kuanzisha tawi hapa tunapenda kuwepo Zanzibar,’’ alisisitiza Prof. Muawia.
Ujumbe huo wa USC ulikutana na viongozi wa SUZA kwenye kampasi ta Tunguu iliyoko Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 19/09/2025, ulifanya pia ziara katika kampasi ya Taasisi ya Utalii iliyoko Maruhubi na Chuo cha Kilimo na Taasisi ya Utafiti (ZALIRI) huko Kizimbani.
Chuo cha Sadat City cha Misri kilianza kutoa taaluma miaka 35 iliyopita na hadi sasa kina Taasisi za utafiti mbili, maabara 20 zilizosajiliwa, kinatoa program za masomo 238 katika kiwango cha elimu ya juu. Zaidi ya wanafunzi 50,000 wanasoma masomo ya shahada ya kwanza wakati wanafunzi wa shahada za juu ni zaidi ya 10,000.