The State University Of Zanzibar

TUNZO ZA WANAHABARI WACHANGA NA WABUNIFU SUZA ZAFANA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndg. Khalid Masoud Waziri amewataka waandishi wa habari nchini kufanyakazi kwa weledi na ubunifu mkubwa ili kuondoa dhana potofu kwa baadhi ya watu wanaona kazi ya uandishi inaweza kufanywa hata na watu wasiokuwa na taaluma.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh.Lela Moh’d Mussa katika ugawaji wa tunzo za waandishi wa habari chipukizi zilizoandaliwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Kilimani wilaya ya mjini.

Ndg. Khalid amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha waandishi wa habari wanatekeleza majukumu yao bila vikwazo vyovyote kwa lengo la kuharakisha maendelo ya nchi na kuhabarisha jamii hivyo ni vyema waandishi kuipenda kazi yao kwa kuipa kipaumbele ili kuondoa dhana potofu kwa jamii.

Aidha amewataka washindi wa tunzo hizo kujitahidi kuendana kasi ya sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa wabunifu katika kazi zao.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Ndg. Salum Ramadhan akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo amesema Wizara inatoa shukrani kwa Chuo cha SUZA kwa uandaaji wa mashindano hayo ambayo yataleta tija na kuzalisha wanahabari bora kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Akitoa hotuba kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA Prof. Mohd Makame Haji. Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Hashim Hamza Chande amesema kuwa uongozi wa chuo unaendelea kuiimarisha Idara ya habari ili kuleta maendeleo kwa kuandaa wanahabari mahiri nchini pamoja na kusema kuwa lengo la mashindano hayo ni kupata wataalamu wenye uwezo wa kutosha katika tasnia ya habari watakaoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuwataka kuepuka kutoa taarifa zitakazoweza kuleta migogoro katika jamii. Hafla hiyo ya ugawaji wa tunzo umefanyika leo 10 Mei, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Balozi mdogo wa China Zanzibar, wanahabari wakongwe wa Zanzibar, viongozi mbalimbali wa SUZA, wafanyakazi na wanafunzi