The State University Of Zanzibar

WANAFUNZI WA SUZA WASHIRIKI MAFUNZO YA KUBADILISHANA UJUZI NCHINI ROMANIA (ERASMUS MOBILITY PROGRAMME)

Wanafunzi 15 kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wamepata fursa adhimu ya kushiriki katika programu ya kimataifa ya kubadilishana Ujuzi (Erasmus Mobility Programme) kati ya SUZA na Chuo Kikuu cha Oradea kilichopo nchini Romania. Programu hiyo inaendeshwa kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kitaaluma na kijamii kati ya vyuo vikuu vya Afrika na Ulaya.

Kabla ya kuanza safari yao ya kitaaluma nje ya nchi, wanafunzi hao walipata mafunzo ya awali kupitia kozi fupi (short course) wakiwa Zanzibar. Kisha walielekea Romania mnamo tarehe 10 Mei 2025, ambapo wanatarajiwa kuhitimisha programu hiyo tarehe 25 Mei 2025. Katika msafara huo wamo pia Wanataaluma watano wanaowasindikiza wanafunzi hao wanaosoma programu mbalimbali zinazotolewa na SUZA.

Lengo kuu la Erasmus Mobility Programme ni kuandaa mazingira ya kubadilishana ujuzi baina ya wanafunzi wa mataifa mbalimbali, pamoja na kuwapa nafasi ya kufahamu mifumo tofauti ya elimu, utamaduni na maisha ya kijamii. Kupitia programu hii, wanafunzi wa SUZA wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo, kujenga uwezo wa kitaaluma na kujiandaa kwa hatua za juu zaidi za elimu, ikiwemo Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (PhD).

Mbali na masomo, wanafunzi hao pia wanajengewa uwezo wa kuwasiliana na kushirikiana na watu kutoka tamaduni na mazingira tofauti, jambo ambalo ni msingi muhimu katika dunia ya leo inayohitaji ushirikiano wa kimataifa.