Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimefanya mazungumzo na Taasisi ya Sayansi za Hisabati ya Afrika (African Institute for Mathematical Sciences – AIMS) tawi la Rwanda, yakilenga kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili katika Nyanja mbalimbali, hususan ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Mazungumzo hayo, yaliyofanyika tarehe 29 Aprili 2025 katika ofisiza makao makuu ya SUZA, Tunguu—Mkoa wa Kusini Unguja—yaliwahusisha viongozi mbalimbali wa SUZA, akiwemo Mkuu wa Skuli ya Elimu, Dk. Said Khamis Juma, pamoja na Dk. Ali Adnan, Mkuu wa Skuli ya Kompyuta, Bibi Najat S. Mohammed, Bwana Ali Mshindo, na Bi Farha, ambao ni wanufaika wa AIMS.
Katika mkutano huo, Rais wa AIMS, Prof. Sam Yala, aliyekuwa ameambatana na Mkurugenzi wa AIMS, Bw. Isambi Sailon, walikubaliana kushirikiana kuinua fani hiyo kwa pamoja.
Maeneo mengine ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni; kubadilishana ziara kati ya wanataaluma ni; kutoa ushawishi kwa wanafunzi wa kike ili waipende Sayansi, kuandaa mijadala ya kitaaluma kuhusu masomo ya Sayansi na hisabati na kuanzisha Shahada ya Uzamili katika somo la Hisabati.
Katika ziara hiyo, Prof. Sam Yala na Bw. Isambi Sailon walipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa mwaka watatu katika fani za Sayansi Asilia na Sayansi ya Kompyuta, wa kiwapa maelezo kuhusu fursa zinazopatikana katika taasisi hiyo, huku wahitimu waliowahi kunufaika na AIMS walitoa ushuhuda wao.
AIMS ilianzishwa mwaka 2003 nchini Afrika Kusini na ina matawi katika nchi mbalimbali, ikiwemo Senegal, Ghana, Cameroon, na Rwanda. Taasisi hiyo imeweka mikakati mahsusi ya kuwawezesha wanafunzi wa kike kujiamini katika masomo ya Sayansi, huku ikitoa ufadhili maalum kwa wanafunzi wa kike wanaosomea fani ya mabadiliko ya tabianchi.