


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ametembelea banda la maonesho la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) lililoonesha huduma mbali mbali zinazotolewa na taasisi za Chuo hiki.
Dk. Mwinyi alipewa maelezo ya shughuli zinazotekelezwa na SUZA ikiwa ni pamoja na masuala ya afya ya binadamu na wanyama, ujasiriamali, taaluma ya ufugaji wa majongoo, ufugaji wa ng’ombe wa wa maziwa, kilimo cha kisasa cha migomba na minazi, uzalishaji wa mayai ya kisasa, ushajiishaji wa upigaji kura kwa amani.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi aliwahutubia wananchi waliohudhuria katika sherehe hiyo na kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora kutoka vyama na taasisi mbali mbali.
Katika hotuba yake, Dk. Mwinyi aliwapongeza wafanyakazi kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuwahimiza kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kutii sheria na kuilinda nchi yenye haki na umoja.
‘’Tunapokwenda kwenye uchaguzi, tufanye uchaguzi wa amani’’, alisisitiza Dk. Mwinyi.
Katika hatua nyengine, SUZA ilikuwa ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki maonesho kwa njia ya magari ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kumsaidia mtu damu, vyombo vya habari, miche ya miungo, ng’ombe ya maziwa.
Maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa Kizimkazi Mkoa wa Kusini tarehe 1/05/2025 yaliongozwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar ambapo yaliwashirikisha wafanyakazi mbali mbali wa taasisi za Serikali na kuwa na ujumbe; Tufanye Kazi kwa Nidhamu na Bidii Tudai Haki zetu kwa Mujibu wa Sheria na Tushiriki Uchaguzi kwa Amani.