The State University Of Zanzibar

MAADHIMISHO YA SIKU YA USTAWI WA WANAFUNZI 2025

SUZA yawaandaa viongozi mahiri

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wanawake na Watoto Mhe. Anna Athanus Paul amesema Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kinawaandaa viongozi mahiri watakaoweza kusimamia mipango na mikakati mikuu ya nchi siku zijazo.


Akitoa hutuba ya maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Wanafunzi yaliyoandaliwa na Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZASO) yaliyofanyika Taasisi ya Utalii huko Maruhubi Kampasi ya SUZA, Mhe. Anna alisema ameridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya SUZASO unaoonesha umahiri na ukomavu kwa viongozi wake.


Alitaja miongoni mwa mambo yaliyomvutia ni uongozi kuunda Wizara Ustawi wa Wanafunzi ili kutoa fursa kwa shughuli zinazohusu ustawi kushughulikiwa na wanafunzi wenyewe badala ya Wizara inayoshughulikia watu wenye ulemavu.


‘’Huu ni ubunifu mzuri na ndio ukomavu wa kimaono wa na huu ndio ushahidi kweli SUZA tunawaandaa viongozi bora na mahiri kupitia SUZASO’’, alisema.

Akizungumzia kuhusu masuala ya udhalilishaji, alisema dhamira njema ya Serikali ya kuzalisha vijana waliobobea katika taaluma haitaweza kufikiwa iwapo vitendo viovu vya udhalilishaji hasa kwa wanawake na watoto vitaendelea kuwepo na kudhoofisha malengo ya utoaji elimu bora.

Vilevile alitoa wito kwa wanafunzi kutokaa kimya iwapo kutakuwa na ishara au matukio udhalilishaji na kuwataka kuripoti kwenye mamlaka zilizowekwa kisheria.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi imejitahidi katika ujenzi wa miundombinu kama vile skuli za kisasa, uimarishaji wa elimu ya juu sambamba na ujenzi wa majengo mapya ya SUZA.


Mapema, Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji alisema SUZA inafanya mambo mengi yenye mnasaba na Siku ya Ustawi kwa kutoa elimu bora kupitia programu zake programu 60 za Cheti, Diploma, Shahada, Digirii na Uzamivu.

‘’Programu zote zinatolewa katika kiwango bora cha kuwawezesha wahitimu kutumia taaluma kuleta mabadiliko na kuchangia maendeleo ya nchi ‘’, alisisitiza Prof. Haji.

Kuhusu kupambana na udhalilishaji, Prof. Haji alisema Chuo kimeweka madawati ya Jinsia katika Kampasi zake zote ambazo zina uwakilishi kwa walimu na wanafunzi kutoa malalamiko yao.


‘’Chuo Kikuu pia kinatoa elimu kwa wanafunzi 58 wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye uoni hafifu, wasioweza kutembea na kuzungumza na wote wanafanya vizuri kutokana na mipango mizuri iliyowekwa ya utoaji wa elimu’’, alikumbusha Prof. Haji.

Mambo mengine ambayo Prof. aliyataja kuwa ni mafanikio katika ustawi wa wanafunzi ni kuwepo kwa bajeti maalum ya Serikali ya Wanafunzi, kuwashirikisha katika kila matukio ya Chuo kama vile vikao vya juu vya SUZA vya kupitisha maamuzi, kuwashirikisha katika matamasha ya michezo ya ndani na nje ya nchi, kuwawekea vituo vya ujasiriamali, kuangalia mahitaji ya karne ya 21 ya Teknolojia ya kisasa na kuwawekea wanafunzi miundombinu hiyo na kituo maaluma cha kuatamia mawazo ya kibiashara.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya SUZA, Mwanamkuu Jega Bakari, aliushukuru uongozi wa SUZA kwa kuwasimamia vyema katika masomo na shughuli zao za Serikali yao sambamba na masomo yao.

Katika hafla hiyo, Rais wa Wanafunzi aliiomba Wizara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee, Wanawake naWatoto kushirikiana nayo kwa kupewa mafunzo yanayohusua masuala ya ustawi wa jamii ombi ambalo mgeni rasmi alilikubali. Naye Waziri wa anayesimamia masuala ya Ustawi wa Serikali ya Wanafunzi, Khatib Nassor alisema kuwa kuwepo kwa Serikali hiyo kumeleta umoja na mshikamano kati ya walimu na wanafunzi wote wa SUZA.